
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imezishauri taasisi na mashirika ya umma nchini kutanguliza uzalendo na maslahi ya umma kwa kununua bidhaa za ngozi zinazozalishwa ndani ya nchi ili kukuza uchumi.
Ushauri huo umetolewa Machi 13, 2026 mjini Moshi na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hawa Mchafu, wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua mradi wa Kiwanda cha Ngozi cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KLICL).
Mhe. Mchafu alisema ni wakati sasa kwa mashirika ya umma na taasisi za serikali kutoa kipaumbele kwa bidhaa za ndani badala ya kuagiza nje, hatua itakayosaidia kukuza viwanda vya ndani na kuongeza ajira kwa watanzania.
"Ni lazima taasisi zetu zionyeshe uzalendo kwa kutumia fedha za walipa kodi kununua bidhaa hizi zinazozalishwa hapa nchini ili kulinda uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali. Hii ndiyo njia pekee ya kukuza uchumi wetu," alisisitiza Mhe. Mchafu.
Mapema, akiwasilisha taarifa ya mradi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, alibainisha kuwa kiwanda hicho kinachomilikiwa na Serikali kupitia Mfuko wa PSSSF na Jeshi la Magereza, kimegharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 142 hadi kukamilika kwake..jpeg)
.jpeg)
Waziri Sangu alieleza kuwa licha ya kiwanda kuanza uzalishaji mwaka 2017 na kuzalisha bidhaa bora, bado kuna changamoto kubwa ya soko la ndani la bidhaa hizo.
"Kiwanda kina uwezo wa kuzalisha hadi jozi milioni 1.2 za viatu kwa mwaka na soli za viatu jozi milioni 2.1. Pia tunazalisha bidhaa nyingine kama mikanda, mabegi na makoti ya ngozi zipatazo 184,500 kwa mwaka, lakini soko letu la ndani bado halijachangamka ipasavyo," alisema Waziri Sangu.
Kufuatia hali hiyo, Mhe. Mchafu aliishauri Wizara na Menejimenti ya KLICL kuwa na mkakati mahsusi wa kutangaza bidhaa hizo kwa kutumia jina la Tanzania ili zivutie masoko zaidi.
.jpeg)
Kwa upande wao, wajumbe wa kamati hiyo akiwemo Mbunge Lucy Kombani na Kafiti W. Kafiti, walipongeza jitihada za PSSSF na kushauri Serikali kuweka utaratibu utakaolazimisha taasisi za elimu na vyombo vya ulinzi na usalama kufanya manunuzi ya viatu katika kiwanda hicho. Waliongeza kuwa kuimarisha soko la ndani kutaifanya PSSSF kupata tija ya uwekezaji huo na kuhakikisha kiwanda kinaendesha kwa faida.
Kamati hiyo ya Bunge inaendelea na ziara yake ya kukagua miradi inayotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ambapo kesho Machi 14, inatarajia kutembelea mradi wa kiwanda cha chai Mponde kilichopo Lushoto mkoani Tanga.
Social Plugin