Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb.), ameielekeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuelekeza mipango na mikakati yake zaidi katika kuendeleza kilimo cha mazao ya chakula na biashara yenye thamani kubwa katika soko la kimataifa, ili kuongeza kipato cha wakulima, wafugaji na wavuvi pamoja na kukuza mchango wa sekta hizo katika uchumi wa taifa.
Aidha, Waziri huyo amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika mazao ya misitu ikiwemo ufugaji wa nyuki, akieleza kuwa sekta hiyo ina fursa kubwa ya kiuchumi na mchango katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu.
Ushauri huo umetolewa leo, Februari 1, 2026, Jijini Dodoma, wakati Waziri wa Fedha alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Frank Nyabundege, ambapo pia alipokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Benki hiyo.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Omar ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na TADB katika utekelezaji wa mikakati yake ya muda wa kati, kwa lengo la kuongeza tija na mchango wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi katika maendeleo ya kiuchumi ya nchi.
Pamoja na hayo, Waziri wa Fedha ameipongeza TADB kwa ufanisi wake wa kiutendaji na mchango wake mkubwa katika kuchochea maendeleo jumuishi na endelevu, hususan katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi pamoja na viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Frank Nyabundege, amesema Benki hiyo imeendelea kukua kwa kasi kifedha, ambapo mizania yake imeongezeka kutoka shilingi bilioni 362.8 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi trilioni 1.3 mwaka 2025.
Bw. Nyabundege amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Benki hiyo mwaka 2015, TADB imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.3 kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, hatua iliyochangia kuimarisha uzalishaji na kuongeza thamani katika mnyororo wa sekta ya kilimo nchini.
Ametoa shukrani kwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuiwezesha Benki hiyo kwa mtaji, akieleza kuwa hatua hiyo inaonesha dhamira na utashi wa kisiasa wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuikuza na kuiendeleza sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji huyo ameiomba Serikali kuendelea kuiwezesha TADB kimtaji kupitia bajeti kuu ya Serikali pamoja na kuidhamini Benki hiyo ili iweze kufikia masoko ya kimataifa ya mitaji, kwa lengo la kuongeza uwezo wa kutoa mikopo kwa wakulima na wadau wengine wa sekta ya kilimo.















Social Plugin