Na Jeshi la Polisi
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura amewataka watanzania wote kushiriki katika jukumu la udhibiti na usimamizi wa Silaha ili kulinda nchi yetu ikiwa ni utekelezaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
IGP Wambura ameyasema hayo Februari 3, 2026 Jijini Dar es Salaam wakati akizindua Kamati ya Udhibiti na Usimamizi wa Silaha pamoja na kufungua Kikao cha kwanza cha Kamati hiyo kinachofanyika kwa siku tatu ambapo zitawasilishwa mada mbalimbali za kuwajengea uwezo wana kamati ili kufahamu majukumu yao, sheria na kanuni,itifaki za kikanda na kimataifa zitakazo waongoza katika jukumu la kudhibiti na kusimamia silaha na risasi nchini.
Amesema, changamoto ya uzagaaji wa silaha haramu kwa kiasi kikubwa ulitokana na migogoro kwa baadhi ya nchi zinazoizunguka Tanzania, kuwepo kwa mipaka isiyo rasmi na ukiukwaji wa sheria.
Aidha, alisema changamoto hiyo ilikuwa kubwa katika miaka ya 2000 kurudi nyuma kutokana na machafuko yaliyokuwa yanaendelea nchi jirani lakini kutokana na kuboreshwa kwa mikakati ya udhibiti na usimamizi wa silaha,tatizo hilo limepungua kutokana na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na vyombo vya usalama.
IGP Wambura alimaliza hotuba yake kwa kutumia maneno ya kizalendo yanayosema kwamba "naapa na ahidi kuendelea kuilinda nchi yangu Tanzania kwa ujasiri mkubwa na kulinda maisha ya Watanzania na mali zao".
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini DCI Ramadhan Kingai amesema udhibiti wa uzagaaji wa silaha nchini umeendelea kudhibitiwa kutokana na mifumo mbalimbali ya usalama iliyopo nchini.
Pia, DCI Kingai ametoa onyo kwa kampuni binafsi za ulinzi ambazo zimekuwa na tabia za kuazimisha silaha wanazotumia katika ulinzi bila kufuata utaratibu kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria na hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa ili kukomesha tabia hiyo.
Naye Mkuu wa Kitengo cha udhibiti wa Silaha, Kamishna Msadidiz wa Polisi (ACP) Bethanema Mlay amesema kwa mujibu wa Sheria ya udhibiti wa Silaha na Risasi ya mwaka 2015 kamati hiyo imeteuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ikijumuisha wajumbe kutoka Tanzania bara na Zanzibar.
Alisema kamati hiyo ni nyenzo muhimu katika kudhibiti silaha nchini ambapo pamoja na majukumu mengine itakuwa na wajibu wa kubaini, kuzuia na kupendekeza namna ya kukabiliana na vihatarishi vilivyopo kuhusiana na uzagaaji wa silaha haramu.

Social Plugin