Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MRADI WA UNDP–GEF WABORESHA UPATIKANAJI WA MAJI NA UMWAGILIAJI KIJIJI CHA SELELA, MONDULI

Na Bora Mustafa - Arusha

Wananchi wa kijiji cha Selela, Kata ya Selela, wilayani Monduli mkoani Arusha, wameushukuru Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) kupitia Programu ya Ruzuku Ndogo inayotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, kwa kufanikisha mradi wa ulinzi wa chanzo cha maji cha Kabambe, ulioboresha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa maji kwa matumizi ya nyumbani na kilimo cha umwagiliaji.

Mradi huo umetekelezwa na Shirika la Waandishi wa Habari la Kusaidia Jamii za Asili (MAIPAC), ikiwa ni sehemu ya mradi wa Kuheshimu na Kulinda Maarifa ya Jamii za Asili katika Uhifadhi (Respecting and Preserving Indigenous Traditional Knowledge in Conservation), ambao pia unatekelezwa kwa jamii ya Wahadzabe katika Bonde la Eyasi, wilayani Karatu.

Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea mradi huo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Selela, Longidonyi Lunda, alisema ujenzi wa uzio wa kulinda chanzo cha maji cha Kabambe umeongeza kiwango cha maji kwa kuondoa uvamizi wa watu, mifugo na wanyamapori katika eneo hilo.

Lunda alisema kwa sasa kijiji kinapata maji ya kutosha kwa matumizi ya binadamu na kwa kilimo cha umwagiliaji, ambapo heka moja sasa humwagiliwa kwa wastani wa masaa manne pekee, ikilinganishwa na zaidi ya masaa sita kabla ya chanzo hicho kulindwa, hali iliyotokana na upungufu wa maji.

Hata hivyo, alisema bado kijiji kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa matanki ya kuhifadhi maji, hali inayosababisha wananchi kupata mgao wa maji kila baada ya siku tatu, na hivyo kuomba ufadhili zaidi ili kuhakikisha upatikanaji wa maji safi ya kunywa muda wote.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mfereji wa Umwagiliaji, Abdallah Side Mbaga, alisema mradi huo umeleta mafanikio makubwa kwa kuwa ulihusisha wananchi moja kwa moja katika utekelezaji wake, jambo lililoimarisha umiliki na uendelevu wa mradi.

“Mwezi huu maeneo mengi yanakabiliwa na ukame, lakini sisi bado tuna maji ya kutosha kwa ajili ya umwagiliaji na matumizi ya wananchi,” alisema Mbaga.

Naye Katibu wa Mfereji huo, Yamini Paulo Mndeme, alisema ujenzi wa uzio na uboreshaji wa mfumo wa usambazaji maji umeongeza uzalishaji wa mazao katika mashamba ya umwagiliaji, hususan ndizi, mbogamboga na matunda, na kuchangia ongezeko la kipato kwa wakulima.

Mkandarasi wa mradi huo, Ephrahimu Samweli, alisema kukamilika kwa mradi kumesababisha ongezeko la maji katika chanzo cha Kabambe, lakini alibainisha kuwa ukosefu wa miundombinu ya kuhifadhi maji ya kunywa bado unasababisha mgao.

“Mimi kama mwanakijiji wa Selela, naishukuru UNDP, GEF, MAIPAC na Serikali kwa mafanikio haya, lakini tunaomba maji ya kunywa yafikie wananchi kwa wingi bila mgao,” alisema.

Wanawake wa kijiji hicho, Ndemta Tumbo na Mary Mollel, walisema mradi huo umeleta nafuu kubwa kwao kwa kuwa sasa wanapata maji kwa urahisi kwa matumizi ya nyumbani na kilimo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la MAIPAC, Mussa Juma, alisema mradi huo unalenga kuongeza kipato cha wananchi kupitia kilimo cha umwagiliaji, sambamba na kulinda na kuhifadhi chanzo cha maji cha Kabambe kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mradi huo ni miongoni mwa miradi 44 iliyotiwa saini tarehe Aprili 4, 2024, katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, chini ya uongozi wa Mwakilishi Mkaazi wa UNDP–Tanzania, Bw. Shigeki Komatsubara, na kuzinduliwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, Isack Joseph, ambaye sasa ni Mbunge wa Jimbo la Monduli.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com