
Wito huu wa kuliombea Taifa na viongozi wake japo umekumbushwa na Dk. Nchimbi kiukweli si jambo la hiari, bali ni agizo kuu la kiroho linalolenga kuhakikisha nchi inabaki katika utulivu na heri.
Katika Biblia katika kitabu cha 1 Timotheo 2:1-2, inasisistizwa kufanyika kwa dua na sala kwa ajili ya wenye mamlaka ili watu waishi kwa amani.Pia mafundisho ya Kiislamu katika Kurani (4:59), inahimizwa utii na kumuombea kiongozi ili apate 'Tawfiq' au muongozo wa Kimungu katika kuwatumikia watu kwa uadilifu.
Tunapomuombea Rais wetu, tunaliombea Taifa letu afya. Biblia inasema katika Mithali 29:2 kuwa 'wenye haki wakiwa na mamlaka, watu hufurahi', hivyo maombi ndiyo yanayofanya wananchi waendelee kufurahia amani na maendeleo .
Mbali na hayo, Makamu wa Rais alikemea mmomonyoko wa maadili na rushwa, akirejea misingi ya imani kuwa mwanadamu anapaswa kuwa mwaminifu. Aliwataka viongozi wa dini kusimamia malezi ya vijana ili kujenga taifa linalomcha Mungu na kuheshimu utu, akisisitiza kuwa "taifa bila maadili ni taifa lililopotea."
Pia, aligusia suala la uhifadhi wa mazingira kama sehemu ya ibada. Alisema kuwa kulinda uumbaji wa Mungu ni jukumu la kila muumini, hivyo akahimiza viongozi wa dini kutumia mimbari zao kukemea ukataji miti na uharibifu wa vyanzo vya maji kwa ajili ya ustawi wa vizazi vijavyo.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa dua maalum kuliombea Taifa, huku Dk. Nchimbi akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kulinda uhuru wa kuabudu na kuhakikisha kuwa amani ya Tanzania inabaki kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika na duniani kote.
Aidha katika kuonyesha kwa vitendo ushirikiano wa Serikali na dini, Dk. Nchimbi alitangaza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa eneo la ekari 12 mkoani Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya CPTC, sambamba na mchango wa Sh. milioni 100 kuanzisha ujenzi huo. Alieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuimarisha taasisi za dini ambazo zimekuwa washirika wakubwa wa serikali katika elimu na afya.
Social Plugin