Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIONGOZI KAHAMA WATAKA UMEME WA UHAKIKA, WAONYA UHUJUMU WA MIUNDOMBINU

  

Na Neema Nkumbi, Kahama

Viongozi wa Wilaya ya Kahama wameitaka TANESCO kuimarisha usimamizi wa miundombinu ya umeme, kuongeza mawasiliano na viongozi wa ngazi za chini pamoja na kuharakisha utekelezaji wa miradi ili kuhakikisha huduma ya umeme inakuwa ya uhakika na endelevu.

Akizungumza leo februari 17, 2026, katika kikao cha TANESCO na wadau kilichofanyika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, Mbunge wa Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, amesema bado kuna changamoto ya baadhi ya nguzo za umeme kuwekwa kwa muda mrefu bila kusimikwa, hali inayosababisha malalamiko kwa wananchi.

Amesisitiza kuwa TANESCO inapaswa kuharakisha usimikaji wa nguzo hizo na kuwashirikisha madiwani inapofanya mabadiliko au kuhamisha miundombinu ili viongozi hao waweze kuwa na taarifa sahihi kwa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Glory Absalum, ameonya juu ya vitendo vya kuhujumu miundombinu ya umeme akisema baadhi ya matukio ya kukatika kwa umeme yanatokana na wizi wa nyaya na uharibifu wa nguzo.

“Wakati mwingine umeme unakatika si kwa sababu TANESCO wamekata, bali tunajihujumu wenyewe kwa kuiba nyaya au nguzo, halafu tunawalaumu TANESCO,” amesema Absalum.

Ameitaka TANESCO kufika haraka kushughulikia hitilafu zinazoripotiwa na kutumia vyombo vya habari kutoa taarifa mapema kuhusu katizo la umeme ili wananchi wote, wakiwemo wasio na simu janja, waweze kupata taarifa kwa wakati.

Naye Meya wa Manispaa ya Kahama, Kaniki, amegusia changamoto ya ukatikaji wa umeme akisema amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi, huku akiwapongeza wahandisi wa TANESCO kwa usikivu wao wanapopewa taarifa za hitilafu.

Katika hatua nyingine, Diwani wa Kata ya Mondo, Kija Peja, ameishauri TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha wanakusanya vifaa vinavyobaki mara baada ya kukamilisha miradi ili kuepusha mkanganyiko na upotevu wa mali za umma.

Amesema kuachwa kwa nguzo au nyaya katika maeneo ya miradi huwafanya baadhi ya wananchi kudhani havina matumizi na hivyo kushawishika kuvichukua.

Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga ameomba ushirikiano wa karibu kutoka kwa madiwani akieleza kuwa wao ndio wako karibu zaidi na wananchi na wanafahamu changamoto zilizopo katika mitaa na vitongoji.

Amesema endapo ushirikiano huo utaimarishwa, hali ya huduma ya umeme itaendelea kuboreshwa zaidi ya ilivyo sasa.

“Madiwani wako karibu na wananchi na wanatambua changamoto zilizopo. Tukishirikiana vizuri, hali tuliyoikuta na ilivyo sasa itazidi kuimarika. Nitaendelea kupokea mawazo, changamoto na ushauri ili tuyafanyie kazi,” amesema Meneja huyo.

Viongozi hao kwa pamoja wamehimiza ulinzi wa miundombinu ya umeme, mawasiliano ya wazi na ushirikiano wa karibu kati ya TANESCO, viongozi na wananchi ili kuhakikisha huduma hiyo inaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya viwanda, biashara na ustawi wa jamii katika Wilaya ya Kahama.

Mwisho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com