NA EMMANUEL MBATILO, BAGAMOYO
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda, amewataka Wathibiti Ubora wa Shule kuhakikisha wanatoa taarifa kwa wakati kuhusu changamoto zinazoikabili sekta ya elimu, ikiwemo ukosefu wa vifaa na madarasa, ili hatua stahiki zichukuliwe haraka.
Akizungumza leo Februari 17, 2026 wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani, wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi ya Wathibiti Ubora wa Shule ngazi ya wilaya, Prof. Mkenda amesema jukumu la wadhibiti hao ni muhimu katika kubaini na kuwasilisha mapungufu yanayojitokeza shuleni.
Amesema Wathibiti Ubora wanapaswa kuwasilisha taarifa hizo kwa Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya ili kuwezesha mamlaka husika kuchukua hatua za haraka za utatuzi.
Aidha, Waziri Mkenda amesisitiza kuwa dhamira kuu ya Wathibiti Ubora wa Shule ni kuhakikisha utekelezaji wa sera, sheria, miongozo na mikakati ya elimu unafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa.
Amewataka watendaji hao kusaidia kikamilifu utekelezaji wa sera za elimu na kuhakikisha wanazielewa kwa undani, hususan sera zinazohusu elimu ya amali na elimu ya lazima.
Akizungumzia mageuzi ya Sekta ya Elimu, Prof. Mkenda amesema kuwa kuanzia mwaka wa masomo 2027/2028, elimu ya msingi itatolewa kwa miaka sita badala ya saba, huku elimu ya lazima ikiongezwa kuwa miaka kumi, kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.
“Mabadiliko haya yataleta ‘double cohort,’ ambapo wanafunzi wa darasa la saba (mfumo wa zamani) na darasa la sita (mfumo mpya) wataingia kidato cha kwanza kwa wakati mmoja. Hata hivyo, hali hiyo ni ya mpito na mfumo utarejea katika ‘single cohort’ baada ya muda,” amefafanua.
Waziri Mkenda ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika shule za ufundi, lakini bado kuna changamoto ya uhaba wa karakana, vifaa na walimu wenye sifa.










Social Plugin