Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIJANA WATAKIWA KUTUMIA UANAGENZI KAMA DARAJA LA KUJIAJIRI


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, ametoa mwito kwa vijana nchini kubadili mtazamo na kutambua kuwa soko la ajira la sasa halihitaji makaratasi pekee, bali linasaka vijana wenye ujuzi mahususi (competence) unaoendana na mahitaji halisi ya kazi.


Kwa mantiki hiyo cheti ni ramani, ujuzi ni gari, yaani cheti kinakuambia unakoenda, lakini ujuzi ndio unaokufikisha.

Akizungumza jijini Dodoma hivi karibuni, CPA Kasore amebainisha kuwa Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 100 katika ujenzi wa vyuo vipya kwenye wilaya 64 na mkoa mmoja, hatua inayolenga kuwapa vijana mahali pa kupata "nguvu ya kitaalamu" ya kushindana duniani.

Amesema kuwa mfumo wa sasa wa VETA umefanyiwa maboresho, ikiwemo kupunguza muda wa masomo na kuanzisha mafunzo kwa njia ya mtandao, ili kuwafikia vijana wengi zaidi hata walio mbali.

“Soko la ajira la sasa linahitaji zaidi ya vyeti. Linahitaji ujuzi unaotatua matatizo. Ndiyo maana tumepanua wigo wa udahili na kuboresha mitaala ili kijana anapohitimu, awe na uwezo wa kuajiriwa, ama muhimu zaidi, awe ameshaandaliwa mazingira ya kujiajiri na kutoa ajira kwa wengine,” alisema CPA Kasore.

Hata hivyo, wakati baadhi ya wadau wakihoji upatikanaji wa soko la ajira, wachambuzi wa masuala ya ufundi wameeleza kuwa mfumo wa uanagenzi ndio dawa ya kuimarisha vyeti vya wahitimu.

Kupitia uanagenzi, kijana hapati tu uzoefu, bali anajenga uaminifu (trust) sokoni ambao unampa uwezo wa kuanzisha karakana au biashara yake mwenyewe badala ya kusubiri milango ya ofisi ifunguke.

Mkurugenzi huyo alihitimisha kwa kusema kuwa maboresho hayo ni sehemu ya Dira ya Taifa 2050, inayolenga kujenga uchumi shindani. Kwa sasa, VETA inasimamia vyuo 80 vyenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 86,000 kwa mwaka, idadi inayotarajiwa kuongezeka mara dufu kufuatia miradi mikubwa ya miundombinu inayoendelea nchini kote.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com