Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA AMLILIA MZEE STEVEN HIZA ALIYETUNGA WIMBO WA 'TANZANIA YETU NDIYO NCHI YA FURAHA'

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameomboleza kifo cha nguli wa muziki wa Tanzania, Steven Hiza, aliyefariki dunia na kuacha pengo kubwa katika tasnia ya sanaa na muziki nchini.

Kupitia salamu zake za rambirambi, Rais Samia amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mzee Hiza, akimtaja kama msanii mahiri na mtunzi wa wimbo mashuhuri wa “Tanzania Yetu Ndiyo Nchi Ya Furaha .” Wimbo huo umeendelea kuwa alama ya uzalendo na umoja wa kitaifa kwa takribani miaka 60, ukiielimisha, kuiburudisha na kuikumbusha jamii wajibu wao kwa Taifa.

Rais Samia amesisitiza kuwa mchango wa marehemu katika sekta ya muziki unatambuliwa na utaendelea kuenziwa, hasa kwa kuwa kazi yake imeendelea kuipamba Tanzania na kuimarisha uzalendo miongoni mwa wananchi wa rika mbalimbali.

Aidha, Rais ametoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu pamoja na wote walioguswa na msiba huo, akiomba Mwenyezi Mungu awape subra na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

“Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina,” amehitimisha Rais Samia katika salamu zake za rambirambi.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com