Wakati dunia ikiendelea kushuhudia mapinduzi makubwa ya kiteknolojia, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas Katambi, ametoa onyo kali dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayoweza kuhatarisha usalama wa Taifa. Akizungumza na maofisa na askari katika Chuo cha Polisi Ziwani, Zanzibar, Katambi amebainisha kuwa teknolojia ni upanga wenye makali mawili: inaweza kujenga uchumi au ikatumika kuchochea machafuko yanayoweza kuligharimu Taifa kwa miongo mingi.
Katambi amegusia ukweli mchungu ambao vijana wengi wanapaswa kuzinduka; kuwa sehemu nyingi duniani zimeingia kwenye vurugu na mipasuko ya kijamii kutokana na habari za uzushi (fake news) na chuki zinazosambazwa kwa kasi ya mwanga kupitia simu za mkononi.
Alisema ni wakati sasa kwa vijana kuacha tabia ya kuwa "mashujaa wa kibodi" (keyboard warriors) wanaoshinda mitandaoni kukosoa bila suluhu, na badala yake wawe mstari wa mbele katika kulinda taswira ya nchi kwa kuitangaza Tanzania na fursa zake badala ya kusambaza picha na video za kudhalilisha utu na amani.
Aidha vijana wanatakiwa kupiga vita upotoshaji kwa kutumia akili na weledi kuchuja taarifa kabla ya kuzisambaza ili kuzuia taharuki na kutumia mtandao kujiajiri na kutatua changamoto za jamii (Agri-tech, Fin-tech) badala ya kugeuza mitandao kuwa kijiwe cha umbea na dhihaka.
Msisitizo wa Waziri Katambi kwa Jeshi la Polisi ni kumbusho kuwa ulinzi wa nchi si wa wenye sare pekee. Jeshi la Polisi linafanya kazi kubwa ya kulinda amani, lakini kijana anayesambaza chuki mtandaoni anadhoofisha juhudi hizo. Uzalendo wa kweli katika karne ya 21 unapimwa kwa jinsi unavyotumia teknolojia kulinda maslahi ya nchi yako.
"Teknolojia isitupumbaze; amani yetu ndiyo mtaji wetu mkuu. Tukichezea mitandao vibaya, tutabaki na simu mkononi lakini nchi ikiwa kwenye magofu," ni fundisho linalopaswa kubaki vichwani mwa kila kijana.
Social Plugin