Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMPUNI ZENYE HISA CHACHE ZAWAKUTANISHA WAKURUGENZI KATIKA MKUTANO WA KIMKAKATI

Serikali imesema Mkutano wa Jukwaa la Wakurugenzi wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Kampuni ambazo ina hisa chache (MIF 2026) utatumika kujadili mbinu za kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi ili kufikia hadhi ya uchumi wa kati wa juu mwaka 2050.

Mkutano huo unaoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), utafanyika Machi 16 hadi 18, 2026 katika Ukumbi wa PAPU, Arusha, ukitarajiwa kuwakutanisha viongozi zaidi ya 150 kutoka kampuni 56 zenye umiliki wa Serikali usiozidi asilimia 51.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini – Mashirika ya Kibiashara, Bi. Lightness Mauki, alisema jukwaa hilo litalenga kuimarisha uongozi na usimamizi wa kimkakati katika kampuni hizo.

Alisema kufikia uchumi wa kati wa juu si jambo la bahati, bali ni matokeo ya maamuzi sahihi, uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali katika mazingira yanayobadilika kwa kasi kiteknolojia na kiuchumi.

Kwa mujibu wake, kaulimbiu ya mwaka huu inalenga kuhamasisha mabadiliko kutoka usimamizi wa kawaida kwenda katika uongozi unaotazama mbele, unaotambua mapema changamoto na kutumia fursa zilizopo kukuza thamani ya uwekezaji.

Tanzania imelenga kukuza uchumi wake hadi kufikia dola trilioni 1 mwaka 2050 kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hatua inayohitaji ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Katika tathmini ya miaka minne iliyopita, thamani ya uwekezaji wa Serikali katika kampuni hizo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 130, mapato ghafi yakifikia zaidi ya Sh10 trilioni huku gawio kwa Serikali likiongezeka kwa kiwango kikubwa.

Bi. Mauki alisisitiza kuwa mafanikio hayo yanatoa matumaini, lakini akabainisha kuwa kasi zaidi, ubunifu na uwazi vinahitajika ili kuhakikisha malengo ya mwaka 2050 yanafikiwa kwa vitendo na si kwa nadharia.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com