Na Bora Mustafa, Arusha.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, ameagiza kuongeza kasi ya ujenzi wa Stendi ya Kisasa inayotekelezwa katika eneo la Bondeni City, Jijini Arusha, ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Akizungumza februari 24,2026 baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Dkt. Nchemba amesema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa hadi sasa.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa mkandarasi anapaswa kuongeza nguvu kazi pamoja na vifaa ili kufidia muda uliopotea kutokana na changamoto za awali, ikiwemo masuala ya fidia.
Mradi huo unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 14.3 na unatekelezwa na kampuni ya Mohammedi Builders Limited, ambayo imeripotiwa kushinda kandarasi za baadhi ya vifurushi vya ujenzi wa kituo cha mabasi na masoko jijini humo.
Kwa sasa, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 49 na unatarajiwa kukamilika mwezi Mei 2026.
Waziri Mkuu amesema Jiji la Arusha ni kitovu cha utalii na biashara katika Kanda ya Kaskazini, hivyo linahitaji miundombinu ya kisasa inayokidhi hadhi yake.
Pia ameeleza kuwa maandalizi ya mashindano ya Africa Cup of Nations yanapaswa kuambatana na maboresho ya miundombinu ya usafiri na barabara ili kulifanya jiji kuwa tayari kupokea wageni na washiriki wa mashindano hayo.
Aidha, amesema ni muhimu kwa Jiji la Arusha kuangalia fursa za miradi ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuhamasisha matumizi ya mabasi yanayotumia nishati safi.
Ametolea mfano wa majiji ya Dar es Salaam na Zanzibar City ambayo tayari yameanza kutumia mabasi yanayotumia gesi, hatua inayochangia kupunguza uchafuzi wa mazingira pamoja na gharama za uendeshaji.
Kupitia mradi huo wa stendi ya kisasa, Arusha inatarajiwa kuboresha huduma za usafiri wa mabasi, kuongeza mapato ya jiji pamoja na kurahisisha shughuli za kibiashara kwa wananchi.

Social Plugin