
Na Hadija Bagasha Tanga,
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, amewahimiza viongozi wa dini na kisiasa kuendelea kuimarisha mshikamano, amani na upendo miongoni mwa jamii ikiwa ni pamoja na kuitaka jamii kusimamia maadili ya vijana kwa misingi ya dini ya Kiislamu sambamba na kuwapatia elimu bora, akisisitiza kuwa hilo ni jukumu la msingi kwa kizazi cha sasa kwa manufaa ya taifa la kesho.
Akizungumza katika kilele cha Maulid Jumuiya kilichofanyika wilayani Pangani, Mkoani Tanga, Makamu wa pili wa Rais amesema wazazi na walezi wana wajibu mkubwa wa kuwalea vijana katika misingi ya ya maadili mema, heshima na nidhamu ili wawe raia wema na wenye mchango mkubwa kwa jamii.
"Niwaombe sana wanatanga tuendelee kudumisha amani na umoja wetu lakini tuendelee kuhakikisha tunasimamia vijana wetu katika maadili mema ya dini yetu lakini tuhakikishe tunasimamia vijana wetu wapate elimu inayostahiki sisi ndio wasimamizi kwasababu kila mchunga ataulizwa kwa alichokichunga tusisahau wajibu wetu wazee wangu hakikishe tunatimiza majukumu yetu mambo ya kheri ni mambo ya kuyakimbilia, akisisitiza Makamu wa pili wa Rais Zanzibar.
Aidha Makamu wa pili wa Rais Zanzibar, alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajabu Abrahman Abdallah, kwa kufanikisha maandalizi ya Maulidi Jumuiya yaliyo wakutanisha waumini na wageni kutoka ndani na nje ya nchi.
Sambamba na hayo Waziri wa Maji na Mbunge wa Jimbo la Pangani, Jumaa Aweso, ameipongeza Serikali kwa ujenzi wa mradi wa barabara ya Tanga–Pangani–Saadani hadi Bagamoyo ambao ametaja kwamba utakuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi, biashara, utalii na ajira kwa wananchi wa Pangani na maeneo ya jirani.
Waziri Aweso pia alieleza mafanikio katika sekta ya uvuvi kupitia upatikanaji wa maboti na vifaa vya kisasa, pamoja na utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Pangani hadi Korogwe wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 175.
Aidha, aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanzisha usafiri wa boti za mwendo kasi kati ya Pangani na Zanzibar, akisema hatua hiyo itaongeza fursa za kiuchumi, kijamii na kiutalii kwa pande zote mbili.
Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa Tanga, Rajabu Abrahman Abdallah, amesema kufanyika kwa tukio hilo Pangani ni heshima kubwa, akibainisha kuwa ni nadra kwa wilaya hiyo kupata fursa ya kutembelewa na viongozi wakuu wa kitaifa katika shughuli za kidini.









Social Plugin