
Na Bora Mustafa, Arusha.
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanahabari ya Kusaidia Jamii za Asili (MAIPAC), umeanza kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari wa Kanda ya Kaskazini na Kati ili kuwajengea uwezo wa kuandika vyema habari za uchunguzi zinazohusu masuala ya mazingira.
Uzinduzi wa mafunzo hayo umefanyika Februari 5, 2026 jijini Arusha, ukiwashirikisha waandishi wa habari 35 kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Singida, Manyara na Dodoma. Mafunzo hayo yanadhaminiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Programu na Uendeshaji wa THRDC, Wakili Halima Sonda, amesema wanahabari wana jukumu kubwa la kuhakikisha dunia na wananchi wanakuwa salama kupitia uandishi wenye tija na uwajibikaji.
Amesema dunia inakabiliwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira, hivyo wanahabari wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha jamii na kuibua masuala yanayohitaji hatua za haraka.
“Lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo wanahabari kuandika kwa weledi habari za mazingira, ikiwemo uchafuzi wa mazingira, ukataji miti na uchimbaji holela wa madini,”
Amesema Wakili sonda .
Pamoja na hayo, akitoa mada kuhusu uandishi wa habari za mazingira, Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma, amesema ni muhimu kwa wanahabari kujikita zaidi katika kuandika masuala ya mazingira kutokana na uhusiano wake mkubwa na haki za binadamu.
Hata hivyo amesema THRDC na MAIPAC zinakusudia kutoa mafunzo kwa wanahabari 140 nchi nzima kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi, ukataji miti, uchafuzi wa mazingira, udhibiti wa taka ngumu, uhifadhi wa mazingira na wanyamapori pamoja na sheria mbalimbali za mazingira na ardhi.
“Baada ya mafunzo haya tuna imani tutakuwa na timu ya waandishi waliobobea katika masuala ya uandishi wa mazingira na uchunguzi,” amesema Juma.
Hata hivyo, amesema bado kuna habari nyingi zinazohitaji uchunguzi wa kina, ikiwemo umuhimu wa matumizi ya nishati safi na kuachana na ukataji miti, uvamizi wa maeneo ya jamii za asili kama Wahadzabe kwa ajili ya kilimo, uchimbaji holela wa madini, matumizi ya kemikali hatarishi pamoja na changamoto ya usimamizi wa taka ngumu.
Aidha, akitoa mada kuhusu sheria mbalimbali za ardhi, mazingira na habari, Wakili Paulo Kisabo amesema masuala ya mazingira yana uhusiano wa moja kwa moja na haki za binadamu.
Amesema wanahabari wanapaswa kuzifahamu sheria za kimataifa na za ndani ya nchi zinazohusiana na haki za binadamu, mazingira pamoja na uhuru wa kujieleza.
“Wanahabari mfanye kazi kwa kuzingatia sheria, kwani mnalindwa na sheria nyingi za ndani ya nchi. Mkizitumia vizuri kalamu zenu, mtalisaidia kwa kiasi kikubwa taifa,” amesema Wakili Kisabo.
Pamoja na hayo, amesisitiza umuhimu wa wanahabari kujifunza sheria mbalimbali kwa manufaa yao, akibainisha kuwa uelewa wa sheria si kwa wanasheria pekee.
Mafunzo hayo yanaendelea jijini Arusha na baadaye yanatarajiwa kufanyika katika kanda nyingine mbalimbali hapa nchini.











Social Plugin