
Na Bora Mustafa, Arusha.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Modest Mkude, ametoa maelekezo kwa viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kuhakikisha wanasimamia kikamilifu suala la usafi wa mazingira sambamba na upangaji wa mji, hususan katika kipindi hiki ambacho Taifa linajiandaa kupokea wageni wa kimataifa kuelekea mashindano ya AFCON, ambapo Jiji la Arusha ni miongoni mwa miji itakayopokea wageni hao.
Mkude ameyasema hayo Februari 7, 2026 wakati wa ziara yake ya kukagua masoko ya Jiji la Arusha, ikiwemo Soko la Kilombero No. 68 pamoja na Soko Kuu la Arusha.
Katika ziara hiyo, amewahimiza wafanyabiashara wote waliopanga bidhaa zao nje ya maeneo yaliyoidhinishwa na Serikali kurejea mara moja katika maeneo yao rasmi ili kupunguza msongamano na kuhakikisha masoko yanakuwa na mpangilio mzuri.
Amesisitiza kuwa nidhamu ya usafi ni jambo la lazima na si hiari, akionya kuwa hakutakuwa na nafasi kwa tabia za uchafuzi wa mazingira, hasa wakati Serikali ikiendelea kuboresha miundombinu ya masoko hayo ili yawe ya kisasa na yenye kuvutia wageni wa ndani na nje ya nchi.
Pia amesema kuwa maandalizi ya AFCON ni fursa kwa Jiji la Arusha kujiweka katika taswira nzuri kimataifa.
Hata hivyo, Mkude amesema mafanikio ya azma hiyo yanahitaji ushirikiano wa kila mmoja, viongozi na wananchi, katika kulinda usafi na mpangilio wa maeneo ya biashara na makazi.
Kwa upande wao, baadhi ya wafanyabiashara katika masoko hayo wameeleza kero mbalimbali zinazowakabili, hususan changamoto za miundombinu, na kuomba Serikali kuendelea kufanya maboresho ili kuwawezesha kufanya biashara katika mazingira bora na kujikwamua kiuchumi.
Aidha, wafanyabiashara hao wameahidi kushirikiana na Serikali kwa kufuata taratibu zote zitakazowekwa, ili kunufaika na fursa za kiuchumi zitakazojitokeza kupitia ongezeko la wageni unaotarajiwa wakati wa mashindano ya AFCON.





Social Plugin