Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BIBI CLOTILDA AMSHUKURU RAIS SAMIA KWA KUOKOA MAISHA YAKE


Na OWM - TAMISEMI, Dodoma

Bibi Clotilda Isidory Kokupima, mkazi wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, amemtembelea Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, na kumuomba awasilishe shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa msaada alioutoa wa Shilingi Milioni 20 kugharamia matibabu ya ugonjwa wa kansa ya utumbo uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu.

Akizungumza na Prof. Shemdoe ofisini kwake, Bibi Clotilda amesema alifika ofisini hapo mahsusi kuomba shukrani zake ziwasilishwe kwa Mheshimiwa Rais, ambaye msaada wake ulimwezesha kupata matibabu katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, hatua iliyookoa maisha yake.

“Ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuokoa maisha yangu. Nilikuwa nikisumbuliwa na ugonjwa wa kansa ya utumbo kwa kipindi cha miaka sita, na matibabu yalisimama baada ya familia yangu kushindwa kumudu gharama. Hata hivyo, baada ya kupata msaada wa Shilingi Milioni 20 kutoka kwa Mheshimiwa Rais, niliweza kuendelea na matibabu,” amesema Bibi Clotilda.

Ameongeza kuwa aliwasilisha barua za maombi ya msaada wa fedha za matibabu kwa wadau wasiopungua kumi, akiwemo Mhe. Rais na ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tangu kuwasilisha ombi lake, alipatiwa msaada huo uliomuwezesha kuendelea na matibabu.

Bibi Clotilda amesema fedha hizo zilimwezesha kukamilisha matibabu katika Hospitali ya Ocean Road na baada ya kumaliza dozi ya mwisho, vipimo vilionesha kuwa hana tena ugonjwa wa kansa uliokuwa ukimsumbua. 

Ameeleza kuwa ameruhusiwa kuendelea na shughuli zake za kila siku, huku akitakiwa kufanyiwa uchunguzi wa afya kila baada ya miezi mitatu.

Aidha, amemshukuru Prof. Shemdoe kwa kukubali kuwasilisha shukrani zake kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa huruma na upendo wake umeokoa uhai wake, na kumuomba aendelee kuwa msaada kwa wananchi wengine wenye uhitaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com