Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBUNGE AZZA HILAL AOMBA BARABARA YA DIDIA–SOLWA IPANDISHWE HADHI 'IWEKWE LAMI', ATAKA TAA TINDE NA NJIAPANDA YA DIDIA


Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hilal Hamad akizungumza katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Shinyanga.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hilal Hamad akizungumza katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Shinyanga.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hilal Hamad akiwa kwenye kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Shinyanga.

Na Kadama Malunde – Malunde 1 Blog

Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hilal Hamad, ameomba Serikali kuipandisha hadhi barabara ya Didia–Solwa ili iweze kuhudumiwa kwa kiwango kinachostahili kulingana na umuhimu wake kiuchumi na kijamii.

Maombi hayo ameyatoa Februari 24, 2026 katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Shinyanga kilichohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mkoa.

Mhe. Azza amesema uboreshaji wa barabara hiyo utarahisisha usafirishaji wa mazao, kuimarisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kufungua fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi wa Didia na Solwa. Sambamba na hilo, ameomba kuwekewa lami kipande cha barabara kutoka njiapanda ya Didia (Puni) hadi Didia Senta ili kuboresha miundombinu ya usafiri na kuchochea maendeleo ya biashara katika eneo hilo.

Ameeleza kuwa Didia Senta inatarajiwa kuwa kitovu muhimu cha uchumi kutokana na ujenzi wa Kituo cha Reli ya Kisasa (SGR), hivyo uboreshaji wa barabara hiyo utawezesha mtiririko mzuri wa watu na mizigo na kunufaisha wananchi pamoja na wawekezaji.

Aidha, amesisitiza kuwa barabara ya Didia–Solwa ikipandishwa hadhi, itaanza kusimamiwa na Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) badala ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), hatua ambayo itaipa uzito wa kitaifa na kuongeza uwezo wa kupata rasilimali za kutosha kwa ajili ya matengenezo na maboresho ya kudumu.

Halikadhalika, Mhe. Azza ameomba pia barabara ya Didia/Kabanga/Mwamalulu kwenda Isakajana katika Jimbo la Msalala ipandishwe hadhi, hatua itakayorahisisha usafiri wa wananchi na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kati ya mikoa na wilaya zinazozunguka eneo hilo.

Katika kuimarisha usalama barabarani, Mbunge huyo pia ameiomba Serikali kuweka taa za barabarani katika njiapanda ya Tinde na Didia pamoja na kufunga taa za kuongozea magari katika njiapanda ya Tinde, kufuatia ongezeko la magari na watembea kwa miguu katika maeneo hayo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuendelea kuimarisha miundombinu ya barabara kupitia Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), huku akitaka usimamizi madhubuti ili kulinda uwekezaji unaofanywa katika sekta hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com