Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Wakazi wa Jiji la Dodoma leo wamejitokeza kwa wingi katika eneo la Nyerere Square kusherehekea kuupokea Mwaka Mpya 2026, huku shamrashamra na furaha zikitawala anga la jiji hilo kuu la Serikali.
Shughuli mbalimbali za burudani, muziki, michezo ya watoto, pamoja na vionjo vya chakula na vinywaji zimetawala katika eneo hilo kuanzia majira ya asubuhi hadi jioni ambapo katika kusherehekea tukio hilo, maeneo ya kandokando ya Nyerere Square yalipambwa kwa taa za rangi jambo lililoashiria kuwa wananchi wanaishi kwa amani.
Jambo hilo limeongeza hamasa kwa wakazi na wageni waliotembelea jiji hilo kwa ajili ya sikukuu.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Malunde Blog wamesema kuwa kuuanza mwaka mpya katika eneo hilo limekuwa tukio la kipekee kwani linatoa fursa ya kuunganisha jamii, kuimarisha undugu na kutoa matumaini ya safari mpya ya mafanikio.
Sherehe hizo zimeendelea kwa amani na utulivu, huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiwa katika uangalizi kuhakikisha kila mkazi anasherehekea katika mazingira salama na rafiki.
Mwaka Mpya 2026 umeanza kwa matumaini mapya kwa wakazi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla, huku wengi wakitamani mwaka huo kuleta maendeleo, neema na mafanikio katika nyanja mbalimbali za maisha.





Social Plugin