Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBUNGE HAPPINESS NGWANDO AADHIMISHA SIKU YA KUZALIWA KWA KUGUSA MAISHA YA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM SONGEA

Mbunge wa viti maalum CCM Ruvuma Happiness Ngwando akiwa anazungumza na waalikwa katika siku yake ya kumbukizi ya kuzaliwa katika ukumbi wa Songea Club Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma leo tarehe Januari 1 2026 pamoja na kula chakula na watoto wanaoishi katika mazingira magumu Songea

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma

Mbunge wa viti maalum CCM Ruvuma Happiness Ngwando, amesema kuwa alikuwa akimuomba Mungu kila siku kwamba akipata nafasi ya kuwa kiongozi ataitumia kuwahudumia watu wenye uhitaji hususani watoto.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati wa kusherehekea siku yake ya kumbukizi ya kuzaliwa iliyofanyika katika ukumbi wa Songea Club, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, mbele ya waalikwa mbalimbali wakiwemo viongozi wa chama na serikali.

Mbunge Ngwando ameshiriki chakula cha pamoja na watoto wenye usonji na yatima kutoka Kituo cha watoto cha RUDEO kilichopo Kata ya Mshangano mkoani Ruvuma, ambapo pia walikata keki kwa pamoja.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed.

Mbunge huyo amewagawia watoto hao mablanketi kwa kila mmoja jumla ya blanketi hayo ni 70 na kuahidi kusimamia ujenzi wa nyumba ya kudumu kwa ajili ya watoto hao, akieleza kuwa kwa sasa wanaishi kwenye nyumba ya kupanga.

Happy Ngwando amesema dunia ina wahitaji wengi na haiwezekani kuwasaidia wote, lakini ataendelea kufanya jitihada kadri Mungu atakavyompa pumzi na afya.

Ameeleza kuwa licha ya kuwa mpole, ni mkali pale ambapo misaada au mahitaji ya watoto hayafikishwi mahali husika, akisisitiza kuwa anachukia matumizi binafsi ya misaada.

Ameongeza kuwa aliomba uongozi ili apate uwanja mpana wa kuwatumikia wananchi na si kwa manufaa binafsi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amempongeza Mbunge Ngwando kwa kitendo hicho cha kugusa maisha ya watoto wenye mahitaji maalum.

Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewatumia salamu za heri ya mwaka mpya na kuhimiza wananchi kuendelea kudumisha amani.

Pia ametoa wito kwa viongozi na wadau kuhakikisha misaada inayotolewa inawafikia walengwa na kuepuka kuitumia kwa maslahi binafsi.

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha watoto yatima cha RUDEO, Edward Ernest, amesema kituo hicho kina watoto 26 wanaoishi ndani ya kituo na watoto 111 wanaoishi nje kwenye familia zao, hivyo kufanya jumla ya watoto 137.

Ameongeza kuwa watoto hao wanatoka wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma na ameishukuru serikali pamoja na wadau kwa kuendelea kushirikiana katika kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalum.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com