
Katika kuelekea mapinduzi makubwa ya usimamizi wa kodi na kuimarisha uchumi wa Taifa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza mkakati mpya wa kuanza kupata taarifa za siri za walipakodi kutoka mataifa mengine.
Akizungumza jijini Dar es Salaam mnamo Januari 23, 2026, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, amebainisha kuwa Tanzania ipo katika hatua za mwisho kujiunga na mfumo wa kubadilishana taarifa za kimataifa moja kwa moja (Automatic Exchange of Information). Mkakati huo unakuja kufuatia kikao cha pamoja kati ya viongozi wa TRA na wakaguzi kutoka Global Forum, wakiongozwa na Mshauri wa Sera za Kodi, Bw. Puneet Gulati.
Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa fedha za umma hazipotei kupitia mifumo ya kimataifa ya ukwepaji kodi. Kamishna Mkuu Mwenda amesisitiza kuwa mfumo huo mpya utaiwezesha TRA kuzibana kampuni kubwa zinazotumia matawi yao ya nje kuficha faida, hali itakayookoa mabilioni ya fedha ambayo hapo awali yalikuwa yakipotea.
Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa kabla ya mwisho wa mwaka 2026, vigezo vyote vya kupata taarifa hizo bila kuomba vimekidhiwa ili kuleta haki na usawa katika mfumo wa kodi.
"Tunataka kutengeneza mfumo wa kodi utakaowezesha kila mmoja kulipa kodi inayostahili, iwe ni mlipakodi wa ndani au wa nje. Hii italeta usawa na kuongeza makusanyo yatakayoiwezesha nchi kuimarisha uchumi na kuleta maendeleo kwa wananchi wake," alisema Bw. Mwenda.
Kwa upande wake, Kamishna wa Walipakodi Wakubwa, Bw. Michael Muhoja, amebainisha kuwa mwelekeo wa sasa wa kiuchumi unataka kila kampuni ilipe kodi kulingana na kiasi cha fedha ilichozalisha ndani ya nchi. Kupitia utaratibu huu wa kimataifa, itakuwa vigumu kwa kampuni yoyote kughushi vitabu vya hesabu ili kuonesha inapata hasara nchini wakati inatengeneza faida kubwa nje ya mipaka ya Tanzania.
Imani ya Kimataifa
Mshauri wa Sera za Kodi kutoka Global Forum, Bw. Puneet Gulati, ameipongeza Tanzania kwa hatua inayopiga kuelekea uwazi wa kodi. Ameeleza kuwa kufuata miongozo na mapendekezo ya kimataifa kutaifanya Tanzania kuwa sehemu ya mfumo wa dunia unaopinga ukwepaji kodi haramu, jambo litakaloongeza imani ya wawekezaji makini wanaozingatia uadilifu.
Hatua hii ya TRA ni sehemu ya mikakati mipana ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha rasilimali za ndani zinatumika vizuri na kila anayepata faida nchini anachangia kodi ipasavyo ili kutoa mazingira tulivu kwa ajili ya uwekezaji na ukuaji wa uchumi wa kitaifa kuelekea Dira ya 2050.
Social Plugin