Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SAUTI ZA WANANCHI: AMANI NDIO MSINGI, TUSIKUBALI KUYUMBISHWA NA MIHEMKO

Wakati Serikali ikiendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini wameendelea kuibuka na kutoa wito wa kudumisha amani, umoja, na mshikamano, wakionya dhidi ya kufuata mihemko na ushawishi wa watu wasiolitakia mema Taifa.

Kutoka mkoani Simiyu, wakazi wa Kijiji cha Mwasubuya wilayani Bariadi wamewataka Watanzania kutumia akili zao wenyewe na kutofanya maamuzi kwa kufuata ya kuambiwa. Pascazia Nocent, mkazi wa kijiji hicho, amesisitiza kuwa utulivu ndio utakaookoa nchi dhidi ya mitego ya watu wabaya.

"Watanzania tutulie, tuache mihemko na tusifuate ya kuambiwa. Tuungane kuijenga Tanzania yenye amani na mshikamano," alisema Pascazia. Kauli hiyo iliungwa mkono na Ngoma Samwel, ambaye aliwaasa vijana kuwa makini na wanaharakati wasio na uzalendo, akiwataka kulilinda Taifa kwa wivu mkubwa.

Mkoani Lindi, Richard Machibya kutoka Nachingwea amekumbusha kuwa pasipo amani, maendeleo hayawezi kupatikana. Alisema kuwa jukumu la kulinda Taifa ni la kila mwananchi ili kuweka mazingira yanayoruhusu ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wa Kilimanjaro, Athumani Saidi, ambaye ni ofisa usafirishaji katika kijiwe cha Lwami, Mwanga, amehusisha amani na imani za kidini. Alisema kuwa amani ndiyo inayoleta uzalendo na utulivu, na kuwataka Watanzania wa imani zote kuliombea Taifa kwani vitabu vya dini vinahubiri amani kama kipaumbele kikuu.

Naye Victoria Mkwizu, mwalimu na mkazi wa Iringa, ametoa tahadhari kuhusu madhara ya vurugu, akibainisha kuwa zikitokea, waathirika wakuu ni akinamama na watoto. "Tunahitaji amani na hatuhitaji vurugu. Ikitoweka tutaishi kwa wasiwasi; tunahitaji utulivu utakaotuletea mshikamano na maendeleo ya jamii," alisema Victoria.

Matumizi ya Mitandao ya Kijamii Akigusia changamoto za teknolojia, Nuhu Ally, fundi ujenzi na mkazi wa Mzumbe, mkoani Morogoro, ametoa ushauri wa kipekee kwa vijana wenzake kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii. Amewasihi vijana kuitumia mitandao hiyo kama fursa ya kujikwamua kiuchumi badala ya kuitumia kama jukwaa la kuhamasisha mambo yanayoweza kuchochea uvunjifu wa amani.

Sauti hizi za Watanzania wa kawaida zinaakisi kiu ya wananchi kuona nchi inabaki kuwa kisiwa cha utulivu, huku wakijiepusha na ajenda za nje zinazoweza kuvuruga mshikamano uliodumu kwa miongo mingi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com