Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAKABIDHI VITABU 5,000 VYA ELIMU YA DINI YA KIISLAMU KWA TISTA


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekabidhi jumla ya vitabu vya Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa Taasisi ya Kusimamia Ufundishaji wa Elimu ya Dini ya Kiislamu (TISTA), ikiwa ni hatua ya kuimarisha ufundishaji wa somo hilo katika shule za sekondari nchini.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo Januari 11, 2026 katika Ofisi za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) jijini Dar es Salaam, ambapo Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mhe. Abubakar Zuberi, ameupokea mzigo huo wa vitabu kwa niaba ya TISTA akiongozana na viongozi wengine wa taasisi hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, amesema wamekabidhi nakala 5,000 za vitabu vya kiada vya somo la Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa kidato cha pili vyenye thamani ya shilingi milioni 16, pamoja na nakala 1,000 za vitabu vya mwongozo wa mwalimu vyenye thamani ya shilingi milioni 1.2, na kufanya jumla ya vitabu vyenye thamani ya shilingi milioni 17.2.

Prof. Mkenda ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuchapa na kusambaza vitabu vya Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa kidato cha sita pamoja na vile vya kidato cha tatu na cha nne mara tu vitakapokamilika, na kuzipa nakala kadhaa BAKWATA kwa ajili ya kusambaza katika shule zisizo za Serikali Tanzania Bara na Zanzibar.

Aidha, ametoa shukrani kwa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kushirikiana kwa karibu na TISTA na kufanikisha zoezi la uandishi pamoja na uidhinishaji wa vitabu hivyo.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu yote ya dini ili kuhakikisha Elimu ya Dini inafundishwa ipasavyo na kuchangia katika kujenga Mtanzania mwenye maadili mema.

Kwa upande wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mhe. Abubakar Zuberi, ameishukuru Serikali kwa ushirikiano uliowezesha uandaaji wa maudhui ya vitabu vya Elimu ya Dini ya Kiislamu, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha malezi na maadili kwa wanafunzi nchini.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com