![]() |
| Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Rajab akizungumza kwenye mashindano ya kitaifa ya kuhifadhi Quran yaliyofanyika Jijini Dodoma January 10,2025 |
![]() |
| Mwenyekiti wa Taasisi ya Riziki Lulida Foundation, Riziki Lulida(Mwenye nguo nyeupe akisikiliza kwa makini mashindano ya Quran Jijini Dodoma |
Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Rajab, ameitaka jamii kuacha kuwatenga watu wenye ulemavu na badala yake kuwapa nafasi sawa katika masuala ya elimu ya dini, akisisitiza kuwa wao ni sehemu kamili ya jamii na wana haki sawa za kujifunza na kutekeleza mafundisho ya dini.
Sheikh Rajab ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika Mashindano ya Kitaifa ya Kuhifadhi Qur’an Tukufu kwa Watu Wenye Ulemavu, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Riziki Lulida Foundation, akieleza kuwa mashindano hayo ni ya kipekee kwa kuwa yanawajumuisha watu ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakisahaulika katika jamii.
Amesema kwa kawaida jamii imekuwa ikiwapuuza watu wenye ulemavu bila kutambua kuwa nao ni binadamu kama wengine, wenye haki ya kusoma, kuabudu na kushiriki kikamilifu katika masuala ya dini, lakini kupitia mashindano hayo, hatua muhimu imechukuliwa kurejesha heshima na nafasi yao katika jamii.
Sheikh Rajab amempongeza Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Riziki Lulida, kwa kuibua wazo hilo la kihistoria, akieleza kuwa ni mara ya kwanza kushuhudiwa kwa mashindano ya aina hiyo kwa ngazi ya kitaifa, jambo ambalo linaonesha ujasiri, maono na moyo wa huruma kwa watu wenye ulemavu.
“Tunakutakia kila la kheri, usichoke siku zote,tunaamini Mwenyezi Mungu ataendelea kukushika mkono kwa kazi hii njema unayoifanya kwa jamii,” amesema Sheikh Rajab.
Aidha, amebainisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatambua na kuthamini Qur’an Tukufu, ndiyo sababu amekuwa akichangia mara kwa mara katika shughuli zinazolenga kukuza mafundisho ya dini na kuimarisha misingi ya maadili katika jamii.
Amesisitiza kuwa watu wote walioshiriki na kuhudhuria mashindano hayo wameonesha kwa vitendo umuhimu wa kuithamini Qur’an Tukufu kama mwongozo wa maisha, akiongeza kuwa amani ni nguzo kuu inayozungumzwa na dini zote duniani.
Kwa mujibu wa Sheikh Rajab, kabla ya kudai haki yoyote, jamii inapaswa kuhakikisha kuwa amani inakuwepo, kwani haki haiwezi kupatikana katika mazingira ya vurugu na machafuko.
Ameonya kuwa uvunjifu wa amani, uchochezi na kuhamasisha vurugu haviendani na misingi ya dini wala mafundisho ya Qur’an.
Amefafanua kuwa haiwezekani kutenganisha amani na Qur’an, kwani vitu hivyo viwili vinaishi pamoja, na waumini wote wanapaswa kuwa walinzi wa amani katika jamii zao kwa vitendo na maneno.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Riziki Lulida Foundation, Riziki Lulida, amesema hakuzaliwa na ulemavu bali aliupata baada ya kupata ajali, akieleza kuwa hali hiyo imemfundisha kuwa mtu yeyote anaweza kuwa mlemavu wakati wowote katika maisha yake.
Ameongeza kuwa endapo vita au machafuko yatatokea, kundi la kwanza kuathirika ni watu wenye ulemavu, jambo linaloonesha umuhimu wa kulinda amani na kuwajali watu wenye mahitaji maalum katika jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Taasisi hiyo mwanafamilia Mariam Lulida, amesema Qur’an Tukufu inakumbusha umuhimu wa kumkumbuka na kumtukuza Mwenyezi Mungu, akisisitiza kuwa yeyote anayemtukuza Mungu ni mtu mtukufu bila kujali hali yake ya kimwili.
Amesema kupitia mashindano hayo ya kuhifadhi Qur’an, jamii inajengwa katika misingi ya haki na usawa, huku ikifundishwa kuwa changamoto, ikiwemo ulemavu, sio mwisho wa matumaini bali ni sehemu ya safari ya maisha inayoweza kuzaa mafanikio makubwa.










Social Plugin