
Na Bora Mustafa, Arusha .
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, amesema kuwa kuwajengea uelewa wa pamoja wanasheria na mawakili wa serikali katika utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi ni utekelezaji wa vitendo wa maono na ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuhakikisha wananchi wanapata haki na kuondokana na changamoto zinazowakabili.
Mhe. Makalla amebainisha hayo Januari 28, 2026, jijini Arusha katika ufunguzi wa mafunzo ya mawakili wa serikali kuhusu utoaji wa msaada wa kisheria. Amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuwatumia mawakili wake katika kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi katika masuala yasiyokuwa na mgongano wa kimaslahi.
Amesema serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kwa ufanisi, pamoja na kuwajengea wanasheria uwezo wa kushughulikia changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakumba wananchi, hasa wale wasiokuwa na uwezo wa kugharamia huduma hizo.
“Niwasihi sana kutumia weledi wenu katika kuwahudumia wananchi, pia tujenge utamaduni wa kujitolea kwa ajili ya wananchi kwani huduma za msaada wa kisheria ni wito. Aidha, yachukulieni kwa uzito mafunzo haya na mtoe maoni yatakayoboresha mfumo wa msaada wa kisheria kwa kuwa bado kuna idadi kubwa ya wananchi wenye uhitaji,” amesema Mhe. Makalla.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Franklin Jasson Rwezimula, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wanasheria wa serikali katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria, utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, pamoja na ushughulikiaji wa mashauri ya ukatili wa kijinsia.
Amesema pia mafunzo hayo yatawasaidia wanasheria hao kuelewa vyema miiko ya utekelezaji wa majukumu yao ili kuhakikisha huduma wanazotoa kwa wananchi zinazingatia maadili, sheria na haki, sambamba na kuongeza imani ya wananchi kwa serikali yao.




Social Plugin