Na mwandishi wetu, Dar
Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametajwa na Wanawake na Mabinti wa Kitanzania kama Kiongozi wa mfano na mwanamke mwenye athari chanya kiasi cha kutoweza kupimika kwa wanawake na mabinti wa Tanzania, Wakimsifu na kumpongeza kwa ujasiri na umahiri wake mkubwa katika kuwaletea maendeleo Watanzania.
Kauli hiyo imebainishwa na Bi. Asina Sancho, Kijana na Mjasiriamali wa Kitanzania, akisema Rais Samia amewapa sababu mabinti wengi ya kuamini kuwa wanaweza kufikia malengo yao na kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika kupambania ndoto zao.
"Mama Samia ametutia nguvu sisi mabinti kuamini kuwa tunaweza kusimama na kutimiza ndoto zetu, hata katika nyakati za majaribio, Mama Samia ametupa nguvu ya kuamini hakuna linaloshindikana. Katika imani pia Mhe. Rais amesemwa katika namna nyingi mbaya na bado amekuwa na imani na kuwasamehe waliomkosea licha ya wao waliomkosea kutotaka msamaha." Amesema Bi. Sancho.
Aidha katika maelezo yake wakati akizungumza na waandishi wa habari hii leo Januari 28, 2026, Sancho amemsifu Rais Samia kwa utekelezaji wake wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini pamoja na maboresho makubwa katika sekta za huduma za kijamii nchini, mambo ambayo ameyatekeleza katika kipindi kifupi cha uongozi wake.
Akizungumzia siku 100 za awali za kipindi cha pili cha Rais Samia, Sancho ameeleza kuhusu utekelezaji wa ahadi yake ya kuanza mchakato wa Bima ya afya kwa wote pamoja na utoaji wa ajira zaidi ya 12, 000 kwenye sekta ya afya na elimu kama alivyokuwa ameahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2025.

Social Plugin