
Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, kijiji hicho kilikuwa kikikabiliwa na uhaba mkubwa wa miundombinu, huku shule yao ikiwa na madarasa matatu pekee yaliyokuwa yakitumiwa na zaidi ya wanafunzi 1,000. Hali hiyo ilisababisha watoto kusoma katika mazingira magumu, jambo lililochochea wananchi chini ya usimamizi wa viongozi wao kuanzisha umoja wa “Kibindu Tunayoitaka” ili kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Kupitia mikutano ya mara kwa mara na michango ya hiari, wananchi hao walifanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 200 ambazo zimeelekezwa katika ujenzi wa miundombinu ya shule, kupata mpya kwa wananchi kuanza na madarasa manne mapya na kuboresha sekta ya afya kwa kuwezesha zahanati ya kijiji hicho kupandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya chenye vifaa na majengo ya kisasa. Hatua hiyo ya awaliya ujenzi wa shule iliivutia Serikali, ambayo iliunga mkono juhudi hizo kwa kutoa kiasi kingine cha shilingi milioni 290 kuendeleza ujenzi wa shule, .
Pamoja na mafanikio hayo katika elimu na afya, wakazi wa Kibindu pia wameimarisha usalama wao kwa kuanzisha ujenzi wa kituo cha polisi. Hatua hiyo imekuja kutokana na ukuaji wa haraka wa kata hiyo yenye wakazi zaidi ya 26,580 kwa sensa ya mwaka 2022 na kijiji cha Kibindu chenyewe kikiwa na wakazi zaidi ya 18,000. Kukiwa na mwingiliano mkubwa wa wageni mbalimbali mbali na wenyeji wao Wazigua, ulinzi madhubuti wa amani na mali zao umekuwa ukifikiriwa.
Akizungumzia mapinduzi hayo, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Bi. Amina, ameeleza kuwa ingawa maisha ya Kibindu yameimarika, bado wanaendelea na jitihada za kuboresha huduma za maji ambazo ni changamoto kubwa kwa sasa. Amebainisha kuwa siri ya mafanikio yao ni amani na mshikamano kati ya wananchi na viongozi wao, jambo ambalo limegeuza kijiji hicho kuwa mfano wa kuigwa kitaifa.
Kwa upande wake, Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze imepongeza ari hiyo ya wakazi wa Kibindu na kuahidi kuendelea kushirikiana nao kwa karibu. Umoja wa Kibindu sasa unaangalia mbele zaidi, ukiwa na malengo ya kuifanya kata hiyo kuwa kitovu cha elimu katika kipindi cha miaka kumi ijayo, huku ukitoa somo kwa maeneo mengine nchini kuwa maendeleo hayaji kwa kusubiri bali kwa kuamua.
Social Plugin