
Katika kipindi hiki ambacho Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kufungua milango ya ushirikiano wa kiuchumi na mataifa mbalimbali, ni dhahiri kuwa ajenda ya ajira kwa vijana imeshika kasi.
Mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, na Balozi wa Tanzania nchini Falme za Kiarabu (UAE), Luteni Jenerali (Mst) Yacoub Mohamed, ni ushahidi tosha wa jitihada hizo. Hata hivyo, ni vyema vijana wakatambua kuwa fursa hizi haziji kwa bahati mbaya, bali ni matokeo ya mazingira murua ya amani, utulivu, na uwajibikaji ambayo nchi yetu imeyajenga kwa muda mrefu.
Inasikitisha kuona kuwa kuna baadhi ya watu na mawakala wa uasi wanajaribu kuwapotosha vijana na kuwataka waende kinyume na nchi yao. Vijana wanapaswa kuwa macho na wasidanganyike na maneno ya uchochezi yanayolenga kuvuruga amani. Lazima ifahamike kuwa hakuna nchi yoyote duniani, ikiwemo UAE, itakayokuwa tayari kuingia mikataba ya ajira na nchi ambayo imetawaliwa na uasi au machafuko ya kijamii. Amani ndiyo inatupa hadhi (Brand) kama taifa, na ndiyo inayompa Balozi wetu ujasiri wa kusimama na kusema kuwa vijana wa Kitanzania ni watu wenye nidhamu na wanaostahili kuajiriwa.
Usimamizi imara wa serikali ambao Waziri Sangu amekuwa akisisitiza ni kinga ya kwanza kwa kijana anayetafuta maisha nje ya nchi. Serikali inapoboresha mifumo ya usimamizi wa mawakala, inalenga kuhakikisha kuwa hakuna kijana anayenyanyaswa au kutapeliwa. Hali hii inawezekana tu pale ambapo kuna utii wa sheria na heshima kwa mamlaka zilizopo. Kijana anayejiingiza katika uasi au dharau kwa mifumo ya nchi yake anajiondoa mwenyewe kwenye mnyororo wa ulinzi wa kisheria na kidiplomasia, jambo ambalo ni hatari sana kwa usalama wake anapokuwa ugenini.
Mazingira ya amani na utulivu ndiyo msingi mkuu unaosababisha mazungumzo ya kidiplomasia kufanikiwa. Tunapopambania amani, tunapambania pia soko letu la ajira. Kila kijana ana wajibu wa kuwa balozi wa amani na kuitunza taswira nzuri ya Tanzania. Kwa kufanya hivyo, tunajenga mazingira ambayo serikali inaweza kuendelea kujadiliana na mataifa mengine kwa ajili ya fursa zaidi. Tuipende nchi yetu, tuheshimu taratibu zilizowekwa, na tujiepushe na mtu yeyote anayehubiri uasi, kwani huyo ni adui wa maendeleo na adui wa ajira za vijana.
Uzalendo na unyenyekevu mbele ya mamlaka si udhaifu, bali ni busara inayohitajika ili kuivusha Tanzania kuelekea katika mafanikio makubwa zaidi. Tushikamane kama taifa moja, tukiunga mkono jitihada za viongozi wetu katika kuimarisha usimamizi na kutoa fursa zenye haki na usawa kwa kila Mtanzania, tukiwa na uhakika kuwa pasipo amani, hakuna maendeleo wala ajira inayoweza kustawi.
Social Plugin