Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ELIMU YA MAJANGA YAPUNGUZA MATUKIO YA MOTO KAHAMA

 

Na Neema Nkumbi

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilayani Kahama mkoani Shinyanga limesema kuwa utoaji wa elimu ya majanga mbalimbali ikiwemo ya moto na maokozi kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari umefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa matukio ya majanga hayo katika jamii ya wilaya hiyo.

Akizungumza Januari 24, 2026 wakati wa mafunzo kwa vitendo yaliyotolewa kwa wanafunzi zaidi ya 100 wa darasa la saba wa Shule ya Mtakatifu Anthony wa Padua, Mkuu wa Kituo cha Zimamoto na Uokoaji wilayani Kahama, Hafidh Omary, amesema elimu hiyo imelenga kuhakikisha usalama wa wanafunzi shuleni na majumbani.

Amesema mafunzo hayo yaliyofanyika katika ofisi za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilayani Kahama ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa jeshi hilo wa kutoa elimu sahihi ya majanga na maokozi kwa wanafunzi katika wilaya hiyo.

Omary amesema kuwa utoaji wa elimu kuanzia ngazi ya chini ni njia sahihi ya kuhakikisha jamii inaelewa na kuzingatia tahadhari za majanga kwa ufanisi zaidi.

“Mwendelezo wa elimu hii kwa wanafunzi katika wilaya yetu ya Kahama ni mpango mkakati ambao tumejiwekea, tunaamini elimu inapofika kuanzia ngazi ya chini inaeleweka kwa usahihi zaidi, samaki mkunje angali mbichi,” amesema Omary.

Ameongeza kuwa kuwapatia wanafunzi elimu0 hiyo mapema huwasaidia kukua wakiwa na uelewa wa namna ya kubaini majanga, kujilinda, kutoa taarifa mapema na kuchukua hatua za awali pale majanga yanapotokea.

Kwa mujibu wa Omary, mpango huo umechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa majanga ya moto yaliyokuwa yakisababishwa na wanafunzi hasa wakati wa likizo wakiwa majumbani pamoja na yale yaliyokuwa yakitokea mashuleni.

“Majanga ya moto yaliyokuwa yakisababishwa na watoto wakiwa majumbani kipindi cha likizo yamepungua sana, hata matukio ya mabweni kuungua mashuleni yamepungua baada ya wanafunzi kufahamu madhara na kujisimamia wenyewe,” amesema.

Ametoa wito kwa walimu kuendelea kuwakumbusha wanafunzi elimu hiyo kwa vitendo ili iendelee kuwajengea kumbukumbu na kuzuia kusahaulika kwa yale waliyojifunza.

Kwa upande wake, Mwalimu wa shule hiyo Joseph Makaka amesema wanafunzi wamepata elimu kwa vitendo na kuahidi kuwa watashirikisha wanafunzi wengine waliobaki shuleni ili kuongeza uelewa kwa wanafunzi wengi zaidi.

Mwanafunzi Amanda Mbago amesema elimu aliyopata itamsaidia katika masomo pamoja na0⁰ kuwa balozi mzuri wa tahadhari za majanga nyumbani.

Naye mwanafunzi Bertness Wilbert ameomba shule kuwezewa ving’amua moshi ili kusaidia kugundua moto mapema, kuuripoti na kuudhibiti kabla haujaleta madhara makubwa.

Wanafunzi hao wamejifunza kutambua majanga katika hatua za awali, huduma ya kwanza, matumizi sahihi ya vifaa vya maokozi, namna ya kutoa taarifa za dharura kwa mamlaka husika pamoja na umuhimu wa kuwa watulivu na kushirikiana wakati wa majanga.



Mwisho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com