Muonekano wa madaraja yaliyojengwa na wakandarasi wazawa katika Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama
Na Neema Nkumbi -Kahama
Serikali imetangaza kuongeza kiwango cha tenda zinazotolewa kwa wakandarasi wazawa hadi kufikia shilingi bilioni 50, hatua inayotokana na uaminifu mkubwa walioujenga kwa kutekeleza miradi kwa ubora na kuikamilisha kwa wakati.
Akizungumza katika ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu ya madaraja yaliyoharibika kutokana na athari za mvua za El-Nino na kimbunga Hidaya, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema serikali imeridhishwa na kazi zinazofanywa na wakandarasi wa ndani katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama.
Mhandisi Kasekenya amesema wakandarasi wazawa wamefanikiwa kujenga madaraja matatu yaliyogharimu zaidi ya shilingi bilioni 13.5 fedha kutoka ufadhili wa Benki ya Dunia, huku miradi hiyo ikifikia asilimia 99 ya utekelezaji.
Amesema maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan yamelenga kuwajengea uwezo wakandarasi wazawa kwa kuwapa tenda kubwa ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa ndani, kwani ajira zinazotokana na miradi hiyo huwanufaisha wananchi wa maeneo husika na fedha huzunguka ndani ya nchi.
“Tunalenga kuona wakandarasi wetu wasiishie kufanya kazi ndani ya nchi pekee, bali waombe na kushinda tenda hata nje ya nchi kwa kuwa tayari wameimarishwa na wana uwezo mkubwa,” amesema Mhandisi Kasekenya.
Ameongeza kuwa hapo awali wakandarasi wazawa walikuwa wanapewa tenda zenye thamani isiyozidi shilingi bilioni 10, lakini kwa sasa serikali imewaamini hadi kufikia tenda za shilingi bilioni 50 kutokana na utendaji wao mzuri.
Kwa upande wa wananchi, wameishukuru serikali kwa ujenzi wa madaraja makubwa uliomaliza changamoto za usafiri wakati wa mvua. Mkazi wa Ushetu, Idd Nkole, amesema daraja la Ubagwe II limeleta nafuu kubwa kwa wananchi.
“Awali tulikuwa tunavushwa kwa mitumbwi, hali iliyokuwa hatarishi. Kwa sasa usumbufu umeisha kabisa, tunaipongeza sana serikali,” amesema Nkole.
Naye Zakaria Bundala amesema daraja la Ubagwe limekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi, akieleza kuwa hapo awali maji yalipofurika walishindwa kuvuka, hali iliyowaathiri hata wajawazito.
“Tuna furaha kubwa kuona daraja hili, tunamshukuru Rais Samia kwa kutuona,” amesema Bundala.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Ntuli Mwaikokesya, amesema miradi yote mitatu imefikia asilimia 99 ya utekelezaji, ambapo kazi kubwa zimekamilika na kinachoendelea ni umaliziaji wa kazi za kulinda madaraja.
Amebainisha kuwa changamoto kubwa wakati wa utekelezaji zilikuwa mvua nyingi zilizosababisha mito kujaa na kupunguza kasi ya ujenzi, lakini kupitia usimamizi wa TANROADS na juhudi za wakandarasi, changamoto hizo zimetatuliwa.
Madaraja yaliyotembelewa ni Daraja la Kasenga lenye urefu wa mita 80, Daraja la Ubagwe II mita 60 na Daraja la Ng’hwande mita 60, yote yakiwa katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama na yamefikia asilimia 99 ya kukamilika.
Social Plugin