Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC MASANJA AONYA UZEMBE AWEKA MKAZO ULINZI NA KASI YA MAENDELEO TUNDURU

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Denis Masanja akiwa anazungumza na madiwani katika baraza la kwanza la  madiwani katika ukumbi wa Skyway Tunduru Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Seif Hassan Dauda akiongoza baraza la kwanza la madiwani katika ukumbi wa Skyway leo Januari 30Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Chiza Marando akizungumza jambo na Mkuu wa wilaya ya Tunduru Mhe.Denis Masanja katika baraza la kwanza la madiwani Tunduru katika ukumbi wa Skyway 

Na Regina Ndumbaro Tunduru-Ruvuma 

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Denis Masanja, amethibitisha kushikiliwa kwa mtendaji wa kata mmoja na jeshi la polisi kwa tuhuma za kuwaruhusu raia watano wa kigeni kuingia wilayani humo bila kufuata sheria na taratibu za nchi. 

Mhe. Masanja ametoa kauli hiyo leo wakati wa ufunguzi wa Baraza la Kwanza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru lililofanyika leo Januari 30 katika ukumbi wa Skyway, akisisitiza kuwa serikali haitavumilia uzembe unaohatarisha ulinzi na usalama wa taifa.

Akizungumza katika baraza hilo, Mhe. Masanja amesema suala la ulinzi na usalama ni jukumu la kila mmoja, hususani kwa wilaya iliyopo mpakani kama Tunduru, na kuwataka madiwani kushiriki kikamilifu katika kuzuia wahamiaji haramu. 

Amesisitiza kuwa viongozi wa ngazi zote wanapaswa kuwajibika na kuchukua hatua mapema ili kulinda amani na usalama wa wananchi.

Kwa upande wa elimu, Mkuu wa Wilaya  huyo ameeleza kutoridhishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi, akibainisha kuwa baadhi ya shule bado zinaendelea kukabiliwa na mazingira magumu ya kujifunzia licha ya fedha kutolewa kwa ajili ya ukarabati wa madarasa chakavu. 

Ametolea mfano shule za msingi Tunduru Mchanganyiko na Majimaji, akisema utekelezaji hafifu umeathiri mahudhurio ya wanafunzi na kuwataka watumishi kusimamia miradi hiyo kwa ufanisi zaidi.

Aidha, Mhe. Masanja amewataka madiwani kusimamia kwa karibu ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri, matumizi sahihi ya fedha za umma na ujenzi wa miradi ya maendeleo, sambamba na kulipa madeni ya watumishi na wazabuni kwa wakati. 

Pia amehimiza utunzaji wa mazingira kupitia kampeni ya kitaifa ya upandaji miti milioni 1.5 wilayani Tunduru, kuwakaribisha wawekezaji na kuhimiza wananchi kulima mazao ya chakula ili kuimarisha ustawi na maendeleo endelevu ya wilaya.Waheshimiwa Madiwani wakiwa wamesimama baada ya wimbo wa taifa kuimbwa kabla ya kuanza kwa baraza hilo la kwanza lililofanyika leo Januari 30 katika ukumbi wa Skyway Tunduru 



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com