Jeshi la Polisi Tanzania limetoa taarifa rasmi kwa umma likiwashukuru wananchi kwa kuonyesha uzalendo na utulivu mkubwa wakati wa kuupokea mwaka mpya wa 2026.
Licha ya kuwepo kwa jitihada za baadhi ya watu kupitia mitandao ya kijamii waliojaribu kuchochea maandamano yenye lengo la kuvuruga amani ya nchi, hali imekuwa tofauti ambapo Watanzania wamepuuza chochezi hizo na kuchagua kusheherekea kwa amani, upendo na utulivu wa hali ya juu.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Kamanda David Misime ameeleza kuwa ushirikiano uliopatikana kutoka kwa wananchi ndio umekuwa nguzo kuu ya kudumisha hali ya usalama nchini kote.
Ingawa hali ya nchi ni shwari, Jeshi la Polisi limesikitika kutangaza vifovya Watanzania kumi mkoani Morogoro kufuatia ajali ya magari mawili yaliyogongana na kuwaka moto.
Hata hivyo, katika nyanja ya usalama wa raia na mali zao dhidi ya fujo na maandamano, nchi imebaki kuwa na utulivu wa kipekee.
Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa Watanzania wote kuendelea na msimamo huo huo wa kulinda amani na kutokubali kuyumbishwa na jumbe za uchochezi zinazosambazwa. Wananchi wanahimizwa kuendelea kuimarisha upendo na usalama wakati huu wa mwendelezo wa sherehe za mwaka mpya huku wakikumbushwa pia kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuwa na udereva wa kujihami ili kuepuka majanga yanayozuilika. Msisitizo mkubwa umewekwa katika kuendeleza mshikamano wa kitaifa ambao umedhihirisha kuwa Watanzania wanathamini amani kuliko vurugu.

Social Plugin