Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Karatu
WANANCHI Kijiji cha Laja katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha wameishukuru TASAF kukubali Mradi wa kupunguza Umaskini (OPEC) kutekelezwa katika Kiji hicho na kutoa fedha kutekelezwa mradi wa ujenzi wa mpya ya Shule ya Sekondari ambao umesaidia wanafunzi kuondokana na changamoto ya kutembea umbali wa kilometa nane kuisaka elimu.
Wakizungumza wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) Shedrack Mziray aliyekuwa akikagua utekelezaji wa mradi huo,wananchi wa Kijiji hicho wamesema kupitia Mfuko huo wamepata shule hiyo ambayo imeondoa changangamoto wanafunzi waliokuwa wanachaguliwa kujiunga Sekondari kutembea umbali mrefu.
Mkazi wa Kijiji cha Laja Christina Lucas amesema wakati shule haijajengwa katika maeneo hayo wanafunzi walikuwa wanateseka haswa watoto wa kike ambao ndio kundi lililokuwa linaathirika kwasababu wanakutana na adha nyingi.
“Uwepo wa shule hii imepunguza utoro usio wa lazima kwasababu kwa vyovyote vile mtoto akitoka nyumbani kilometa nane njiani anakutana na changamoto nyingi ,mara nyingine wanasindikizwa na bodaboda ambao baadhi yao ni hatari kwa usalama wa wanafunzi Wetu.
“Baada ya kupata mradi huu na shule kujengwa hivi sasa watoto wanakaa katika mabweni hivyo wanakuwa salama na ndio maana mpaka sasa hakuna mwanafunzi ambaye amepata ujauzito kwani wazazi tunafuatilia sana ,watoto wako salama.
Kuhusu TASAF amesema wananchi wa Kijiji cha Laja wanaipongeza na kuishukuru lakini wanatoa ombi la kujengewa majengo ya maabara pamoja na kuongezwa nyumba za walimu kwani zilizopo hazitoshi.
“Tunatamani kama itawezekana basi Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan kupitia TASAF atuone tena kwa kutujengea Maktaba,mabweni na nyumba za walimu.Pia namshukuru Rais wangu kwa kuliona hili kwani hii shule hatukutegemea ingejengwa katika maeneo haya.
“Rais wetu ni msikivu ameangalia mpaka huku kwetu ambako tulisahaulika lakini sasa ametujengea shule ya kifahari ambayo pengine ilitakiwa ijengwe hata Karatu ila kwa sasa iko kijijini kwetu.”
Kwa upande wake Andrea Mtupa amesema wanafunzi wanaofaulu kwenda kidato cha kwanza walikuwa wanatembea umbali wa kilometa nane kwenda na kilometa nane wakati wa kurudi kila siku lakini hivi sasa TASAF kupitia mradi wa OPEC wamejengewa shule ya Sekondari ya kisasa.
Awali Ofisa Mtendaji Kijiji cha Laja Daniel Mpigachai amesema mradi wa ujenzi wa shule hiyo umegharimu Sh.774,946,675, ambapo TASAF kupitia OPEC awamu ya Nne walitoa fedha Sh. 659,505,275 na fedha Sh.115,441,400 ni mchango wa jamii ambao umejumuisha mchanga,Kokoto ,mawe,maji na nguvu kazi wakati wa ujenzi.
Kuhusu manufaa ya mradi amesema shule hiyo iliyosajiliwa Novemba 2023 ilianza rasmi mwaka 2024 kwa kupokea wanafunzi 26 wa Kidato cha kwanza, kwa sasa shule ina Jumla ya wanafunzi 63 ambao ni kidato cha kwanza na cha pili na wote wanakaa Bweni.
“Uwepo wa mradi huu umeondoa tatizo la utoro shuleni, wanafunzi kuongeza morali ya kusoma tofauti na awali walipokuwa wanasoma shule ya kata iliyo na umbali wa Zaidi ya kilometa 8 kutoka kijini kwetu, shule imepokea pia watoto wanaotoka viji vya jirani.
Aidha amesema kwa niaba ya Wananchi wa Kijiji cha Laja wanatoa ombi kwa TASAF kama fursa nyingine itajitokeza wanaomba mradi wa ujenzi Majengo mengine yaliyosalia kama Maabara, Maktaba, Nyumba nyingine za walimu na Madarasa.
Wakati huo huo Mkuu wa Shule ya Sekondari Laja Daniel Panga amesema shule hiyo iliyojengwa kisasa mbali kuondoa changamoto wanafunzi kutembea umbali mrefu imeleta hamasa kwa wanafunzi wanaosoma elimu ya msingi wanaamini ipo siku watajiunga na shule hiyo.








Social Plugin