Katika mitaa ya Maili Moja Kibaha mkoani Pwani hadi kwenye masoko ya Bariadi mkoani Simiyu, sauti za Watanzania wa kada mbalimbali zinaungana katika nukta moja: Amani si jambo la bahati mbaya, ni tunda la malezi na mazingira rafiki. Fundi magari wa Maili Moja, Frimatus Mtenga, anatoa darasa la msingi kwa wazazi. Anasema kuwa jukumu la kwanza la mzazi ni kumfundisha mtoto kutunza amani na kukataa kufuata mkumbo wa vurugu. Kwa mujibu wa Mtenga, mshikamano ndiyo ngao inayomfanya kijana aweze kushika bisibisi au spana yake na kufanya kazi bila hofu, akijiletea maendeleo yake na taifa kwa ujumla.
Umuhimu wa amani unajidhihirisha zaidi pale inapopotea. Malugu Nkwabi, mkazi wa Bariadi, anakumbusha machungu ya vurugu za uchaguzi ambapo walilazimika kufunga biashara saa 12:00 jioni. Maisha hayo ya 'shuruti' si tu yanakosesha kipato, bali yanavuruga utaratibu wa kijamii. Hata kama vurugu zimetokea mkoa mmoja, athari za kiuchumi na kisaikolojia zinasambaa nchi nzima kama donda ndugu.
Amina Mwinyimvua, kiongozi wa soko la Loliondo Kibaha, anasisitiza kuwa amani haina mbadala. Anatoa wito kwa vijana kuachana na ushawishi wa vurugu kwani Watanzania hawakuzoezwa kuishi katika mitafaruku. Utulivu ndio unaomwezesha mama ntilie, muuza samaki, na kijana wa bodaboda kufanya shughuli zao masaa 24 bila wasiwasi.
Kwa kuwa mwanga wa matumaini unaonekana kupitia teknolojia, vijana pia wameelezana kutulia ili kuwa na nafasi ya kufuatilia fursa mbalimbali za maendeleo zinazotolewa na mitandao, kunapokuwa salama kila kitu kinawezekana lakini kuwa na ghasia fursa nyingi zinapotea.
Serikali na wadau wa maendeleo wanahimizwa kuoanisha juhudi hizi za maendeleo kwa kuimarisha amani kupitia malezi ya nyumbani, na kisha kutoa mazingira ya kiufundi na kisera yanayomuwezesha kijana mstaarabu kuneemeka kiuchumi.
Maendeleo ya Tanzania yamefungwa kwenye kifurushi cha mambo mawili: Utulivu wa kijamii na Uwezeshaji wa kiuchumi. Wazazi wanapojenga misingi ya amani, na Serikali inapojenga mazingira rafiki ya biashara, tunatengeneza taifa la vijana walio imara kifikra na kiuchumi. Kama walivyosema wadau wa Kibaha na Bariadi, amani ndiyo kila kitu, na ulinzi wake huanzia ngazi ya familia.
Social Plugin