Na Michael Abel.
Vilio na majonzi vimetawala miongoni mwa wakazi wa Kata ya Ntuntu, wilayani Ikungi mkoani Singida, wakati wa mazishi ya Grace Hamis (32), aliyefariki dunia baada ya kujinyonga usiku wa kuamkia Januari 2, 2026.
Marehemu Grace, inadaiwa alifikia uamuzi huo muda mfupi baada ya kususa sherehe za Mwaka Mpya zilizokuwa zimeandaliwa nyumbani kwa dada yake, hali iliyoacha simanzi kubwa kwa familia, ndugu na wakazi wa eneo hilo.
Akizungumza wakati wa mazishi hayo, Mbunge wa Jimbo la Ikungi Mashariki, Thomas Mgonto, amewataka wananchi kuacha tabia ya kuhukumu familia ya marehemu na badala yake washirikiane nao kwa karibu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida, SACP Amon Kakwale, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha kifo hicho kinahusishwa na msongo wa mawazo.
Jeshi la Polisi limeendelea kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa mapema wanapobaini dalili za msongo wa mawazo au changamoto za kisaikolojia kwa watu wanaowazunguka, ili hatua stahiki zichukuliwe na kuzuia matukio kama haya kujirudia.

Social Plugin