Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMPUNI YA AIRTEL YAZINDUA MNARA WA MAWASILIANO KATA YA NGOKOLO - SHINYANGA

Na Michael Abel

Kampuni ya simu ya Airtel imeendelea kuimarisha huduma za mawasiliano katika Mkoa wa Shinyanga kwa kuzindua mnara mpya wa mawasiliano katika hatua inayolenga kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha huduma za kimtandao kwa wakazi wa mkoa huo.

Uzinduzi huo umefanyika leo katika Mtaa wa Majengo Mapya kata ya Ngokolo ndani ya Manispaa ya Shinyanga ukiibua faraja kubwa kwa viongozi wa serikali za mitaa pamoja na wananchi, ambao kwa muda mrefu walikabiliwa na changamoto ya mawasiliano hafifu, hasa wakati wa matukio ya dharura na uhalifu.

Akizungumza katika tukio hilo, Mtendaji wa Kata ya Ngokolo, Adelaida Abyabato, amesema kuwa awali viongozi na wakazi walikuwa wanapata shida kubwa ya kuwasiliana na vyombo vya dola pindi matukio ya uhalifu yalipotokea, hali iliyosababisha kuchelewa kwa msaada na hatua za kisheria. Ameeleza kuwa uwepo wa mnara huo ni suluhisho muhimu kwa usalama na ustawi wa jamii.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo Mapya, Phelemon Chikala, amesema kuwa kuboreshwa kwa mawasiliano kutasaidia kuimarisha ulinzi na usalama, pamoja na kurahisisha utoaji wa taarifa muhimu kwa wananchi na viongozi kwa wakati.

Baadhi ya wakazi wa eneo hilo wamesema maboresho ya mawasiliano yameleta mabadiliko chanya katika maisha yao ya kila siku. Elizabeth Itete, mkazi wa Mtaa wa Majengo Mapya, amesema kuwa kwa sasa wanaweza kufanya shughuli zao za kiuchumi bila vikwazo vya mawasiliano, huku Eunice Kisija akieleza kuwa huduma bora za mtandao zimewawezesha kuwasiliana kwa urahisi na kufanya biashara kwa njia ya kidijitali.

Meneja wa Kampuni ya Airtel Mkoa wa Shinyanga, George Michael, amesema kampuni hiyo ilipokea malalamiko mengi kutoka kwa wateja wake kuhusu kusuasua kwa mawasiliano katika eneo hilo, jambo lililosababisha kuchukua hatua za makusudi za kuondoa changamoto hiyo. Ameongeza kuwa Airtel itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha huduma bora na endelevu kwa wateja wake.

Uzinduzi wa mnara wa mawasiliano Ngokolo unatarajiwa kuongeza kasi ya shughuli za kiuchumi katika sekta mbalimbali ikiwemo madini, ufugaji na kilimo, sambamba na kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii na kiusalama kwa wakazi wa Manispaa ya Shinyanga.


Mgeni rasmi ambaye ni Mtendaji wa Kata ya Ngokolo Bi. Adelaida Abyabato akizindua mnara huo wa mawasiliano.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com