Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAIPONGEZA JAMBO GROUP KWA KUCHOCHEA VIWANDA, AJIRA NA MASOKO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, pamoja na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya, wakionesha bidhaa za maziwa zinazozalishwa na Kiwanda cha Jambo wakati wa ziara yao ya kikazi . Picha na MALUNDE
Mkurugenzi Mtendaji wa Jambo Group, Mhe. Salum Khamis akieleza hatua za uzalishaji pamoja na uwekezaji uliofanyika kiwandani.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya, ametembelea Kiwanda cha Jambo Group of Companies mkoani Shinyanga na kuipongeza kampuni hiyo kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya viwanda, utoaji wa ajira na upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa wakulima na wafugaji.

Dkt. Chaya amefanya ziara hiyo leo Ijumaa Januari 9,2026 akiwa ameambatana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa na Meneja wa Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi na Maeneo ya Viwanda Tanzania (TISEZA) Kanda ya Ziwa , Phina Jerome na viongozi mbalimbali ambapo wamejionea shughuli za uzalishaji na mifumo ya uendeshaji wa kiwanda hicho kinachojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za matumizi ya kila siku (FMCG), kinachomilikiwa na mwekezaji wa Kitanzania.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Chaya amesema mwelekeo wa Serikali kwa sasa umejikita zaidi katika kuimarisha uwekezaji wa viwanda, kwa lengo la kuhakikisha wakulima na wafugaji wanapata masoko ya uhakika ya mazao yao na kunufaika ipasavyo kupitia ongezeko la thamani.

“Tanzania ina wakulima na wafugaji wengi, lakini changamoto kubwa imekuwa ni masoko ya uhakika na viwanda vya kuchakata mazao. Serikali inahitaji wawekezaji kama Jambo Group wanaowekeza kwenye viwanda vinavyowagusa wananchi moja kwa moja,” amesema Dkt. Chaya.
Naibu Waziri huyo ameipongeza Jambo Group kwa kuajiri wafanyakazi zaidi ya 1,000 wa kudumu na takribani 10,000 wa muda, akisema mchango huo ni mkubwa katika kupunguza tatizo la ajira, hususan kwa vijana na wanawake, na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Aidha, amewahimiza wawekezaji wengine wa Kitanzania kuiga mfano wa Jambo Group, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji ili viwanda viendelee kukua, kuongeza uzalishaji na ajira kwa manufaa ya wananchi, hususan wa Kanda ya Ziwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amewasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kueleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutekeleza ahadi zake kwa vitendo kupitia uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na viwanda.
Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa

Dkt. Kakurwa amesema ameridhishwa na maendeleo yaliyofikiwa na Jambo Group, akisisitiza kuwa Serikali iko tayari kushirikiana na wawekezaji na kutatua changamoto zao ili kuwezesha ukuaji endelevu wa sekta ya viwanda.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amesema uwepo wa Jambo Group mkoani humo ni fahari kubwa na ushahidi kuwa Shinyanga ni eneo salama na rafiki kwa uwekezaji.

Amebainisha kuwa kiwanda hicho kimeongeza ajira, kipato cha kaya na mzunguko wa fedha katika maeneo ya vijijini na mijini.

Akisoma taarifa fupi ya kampuni hiyo, Mkurugenzi wa Jambo Group of Companies, Khamis Salum, amesema ziara ya viongozi wa Serikali ni heshima kubwa na ishara ya dhamira ya Serikali ya kuendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kujenga uchumi imara na shindani.

Ameeleza kuwa Jambo Group ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa katika sekta ya viwanda na bidhaa za matumizi ya kila siku (FMCG), ikiwa imewekeza katika mitambo ya kisasa ya viwango vya Ulaya ili kuhakikisha uzalishaji wenye ufanisi, ubora wa juu na usalama wa bidhaa.
Mkurugenzi wa Jambo Group of Companies, Khamis Salum

Ameongeza kuwa kampuni hiyo ni miongoni mwa walipa kodi wakubwa nchini na imeajiri zaidi ya wafanyakazi 1,000 moja kwa moja pamoja na kutoa ajira zisizo za moja kwa moja kwa zaidi ya watu 10,000 kupitia mnyororo wa thamani, huku miradi yake ya maziwa yenye uwezo wa kuchakata hadi lita 100,000 kwa siku ikitoa soko la uhakika, bei za ushindani, malipo kwa wakati na mafunzo ya ufugaji wa kisasa kwa wafugaji, hivyo kuongeza kipato chao na kuchochea maendeleo ya sekta ya mifugo nchini.

Amesema kupitia vituo vya kukusanyia maziwa vilivyosambaa katika vijiji na miji midogo, Jambo Group imewezesha wafugaji kupata soko la uhakika na endelevu la maziwa yao kila siku, hali iliyopunguza upotevu wa mazao, kuondoa hofu ya kukosa wanunuzi na kuongeza kipato cha kaya.

Aidha, ameeleza kuwa, kampuni hiyo imejenga mifumo rasmi ya ununuzi na malipo kwa wakati inayowezesha utoaji wa bei za haki kulingana na ubora na kiasi cha maziwa, huku ikiendelea kutoa mafunzo ya ufugaji wa kisasa, lishe bora ya mifugo, usimamizi wa malisho, pamoja na kinga na tiba ya magonjwa ya mifugo kwa kushirikiana na wataalam, hatua inayoongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa maziwa na kuimarisha ustawi wa wafugaji na jamii kwa ujumla.

Katika ziara hiyo, Dkt. Chaya pia ametembelea Kiwanda cha Uzalishaji wa Vinywaji Vikali cha East African Spirits (T) Limited (EASTL) pamoja na Kiwanda cha Nyama kilichopo Old Shinyanga, ambapo alisema eneo hilo lipo wazi kwa uwekezaji na kuwataka wawekezaji kujitokeza kuwekeza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jambo Group, Mhe. Salum Khamis, akieleza mchango wa kiwanda hicho katika uundaji wa ajira, ulipaji wa kodi na kukuza maendeleo ya sekta ya maziwa, wakati wa ziara ya viongozi wa Serikali mkoani Shinyanga 
Mkurugenzi Mtendaji wa Jambo Group, Mhe. Salum Khamis, akieleza mchango wa kiwanda hicho katika uundaji wa ajira, ulipaji wa kodi na kukuza maendeleo ya sekta ya maziwa, wakati wa ziara ya viongozi wa Serikali mkoani Shinyanga
Mkurugenzi wa Jambo Group, Khamis Salum, akisoma taarifa fupi ya kampuni hiyo leo Ijumaa, Januari 9, 2026, wakati wa ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi pamoja na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, katika kiwanda hicho.

Mkurugenzi wa Jambo Group, Khamis Salum, akisoma taarifa fupi ya kampuni hiyo leo Ijumaa, Januari 9, 2026, wakati wa ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi pamoja na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, katika kiwanda hicho.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya, akisisitiza umuhimu wa uwekezaji wa viwanda katika kuwasaidia wakulima na wafugaji kupata masoko ya uhakika na endelevu
Mkurugenzi Mtendaji wa Jambo Group, Mhe. Salum Khamis, akiwaongoza viongozi wa Serikali na Mkoa wa Shinyanga kutembelea maeneo mbalimbali ya kiwanda hicho, akieleza hatua za uzalishaji pamoja na uwekezaji uliofanyika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jambo Group, Mhe. Salum Khamis  akieleza hatua za uzalishaji pamoja na uwekezaji uliofanyika kiwandani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jambo Group, Mhe. Salum Khamis  akieleza hatua za uzalishaji pamoja na uwekezaji uliofanyika kiwandani.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, akizungumza wakati wa ziara ya kikazi katika Kiwanda cha Jambo Group, mkoani Shinyanga, akisisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wawekezaji
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, akizungumza wakati wa ziara ya kikazi katika Kiwanda cha Jambo Group, mkoani Shinyanga, akisisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wawekezaji



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com