Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MILIONI 675 KUBORESHA HUDUMA ZA TIBA MANISPAA YA TABORA




Na OWM - TAMISEMI, Tabora

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amesema Serikali imetoa Shilingi Milioni 675 kutekeleza mradi wa ujenzi na upanuzi wa Kituo cha Afya Mailimoja cha Manispaa ya Tabora, ili kuboresha huduma za utoaji tiba kwa wananchi zaidi 45,107 wa kata ya Ipuli katika manispaa hiyo.

Prof. Shemdoe amesema hayo, akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi  na upanuzi wa Kituo cha Afya cha Mailitano kilichopo kata ya Ipuli Manispaa ya Tabora.

“Tumeleta hapa Shilingi Milioni 675, majengo ambayo tumepanga kuyajenga ujenzi umeshaanza na yako katika hatua nzuri, hata mkitazama kwa mbali majengo ya OPD, IPD, LAUNDRY na XRAY yanaonekana kwa macho,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Aidha, Prof. Shemdoe amesema kuwa kuna majengo mengine kama ya Incenerator na Placenta Pit utekelezaji wake haujaanza, majengo ambayo wamepewa wakandarasi wengine na inasemekana wameenda kuanza ujenzi wa miradi katika mikoa mingine, hivyo amemuelekeza Mkuu wa Mkoa kufanya ufuatiliaji ili majengo yote yakamilike.

“Namuelekeza mkandarasi tuliyempa kandarasi aje mara moja kuanza kazi ya ujenzi wa jengo incinerator, Placenta Pit na Ash Pit kwa mujibu wa mkataba, na akichelewa mkataba wake uangaliwe kama unakipengele cha kumkata gharama za ucheleweshaji mradi na akatwe,” amesema Prof. Shemdoe.
 
Prof. Shemdoe ameongeza kuwa, Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inataka ujenzi ukamilike ili wananchi waanze kupata huduma, na ndio maana ilitoa fedha hizo za ujenzi na ukarabati wa Kituo cha Afya Mailitano.

Sanjali na hilo, Prof. Shemdoe ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Tabora kwa kuelekeza ujenzi wa barabara ya Mailitano yenye urefu wa kilomita 2.418 iliyokamilika kwa asilimia 99, barabara ambayo ni fungamanishi katika kuwawezesha wananchi kufika kwenye Kituo cha Afya Mailimoja ili kupata huduma za matibabu.

“Mliokuwa mnakuja kupata huduma kipindi cha nyuma, barabara hii haikuwa nzuri na kipindi cha mvua ilikuwa ni changamoto kufika kwenye kituo hiki cha afya, lakini leo hii hata inyeshe mvua ya mawe kama una mgonjwa utaweza kumfikisha hapa ili auhudumiwe,” amefafanua Prof. Shemdoe.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Kituo cha Afya Mailimoja, Mganga Mfawidhi Dkt. Josephat Mtambalike amesema kuwa, kituo kinahudumia wananchi wote wanaotoka ndani na nje ya Manispaa ya Tabora na kilianza kutoa rasmi huduma mwaka 2018.

Dkt. Mtambalike amesema huduma zinazotolewa katika kituo hicho  ni huduma ya kliniki ya baba mama na mtoto, huduma ya wagonjwa wa nje, huduma ya kulaza wagonjwa, huduma ya kliniki ya kifua kikuu na VVU, huduma ya kinywa na meno, huduma ya upasuaji wa dharura kwa wajawazito wenye changamoto wakati wa kujifungua na huduma za maabara.

Utekelezaji wa mradi wa ujenzi na upanuzi wa Kituo cha Afya Mailimoja unaolenga kuboresha utoaji wa huduma za matibabu kwa wananchi wa Manispaa ya Tabora,  ulianza rasmi Agosti 23, 2025 na unatarajiwa kukamilika Machi 30, 2026.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com