Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI SANGU AAGIZA HATUA KALI KWA WAAJIRI WANAOKWEPA KUWASILISHA MICHANGO NSSF



*Awataka kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati

Na MWANDISHI WETU

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amewaagiza viongozi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya waajiri wa sekta binafsi wanaoshindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati, akisisitiza kuwa kitendo hicho kinawanyima wafanyakazi haki zao za msingi ikiwemo mafao ya uzeeni.

Mhe. Sangu alitoa maelekezo hayo tarehe 17 Desemba 2025 wakati wa ziara yake ya kikazi katika Ofisi za NSSF jijini Dodoma, ikiwa ni ziara yake ya kwanza NSSF tangu alipoteuliwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Katika ziara hiyo, aliambatana na Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Rahma Kisuo.

Alisema kuwa ni wajibu wa kisheria kwa kila mwajiri wa sekta binafsi kujiandikisha katika Mfuko, kuwaandikisha wafanyakazi wake na kuwasilisha michango yao kwa wakati kila mwezi. Waziri huyo alisisitiza kuwa Serikali haitavumilia uzembe au makusudi ya kukiuka sheria kwa waajiri wanaohatarisha mustakabali wa wafanyakazi wao.

“Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, hakikisha waajiri wote wasiowasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati wanachukuliwa hatua za kisheria bila muhali, kwani wanaposababisha kucheleweshwa kwa mafao, huwaumiza wafanyakazi waliolitumikia taifa kwa muda mrefu,” alisema Mhe. Sangu.

Aidha, Waziri huyo aliipongeza NSSF kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, akitaja ongezeko la wanachama na waajiri, kuimarika kwa makusanyo ya michango, mapato ya uwekezaji, kuongezeka kwa thamani ya Mfuko pamoja na maboresho ya malipo ya mafao kwa wanachama.

Akitoa taarifa ya utendaji wa Mfuko, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano kinachoishia tarehe 30 Juni 2025, Mfuko umeongeza idadi ya wanachama wapya kutoka 215,693 mwaka 2020/21 hadi 363,925 mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 68.72.

Aliongeza kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26, Mfuko uliandikisha wanachama wapya 111,881, sawa na asilimia 110 ya lengo, huku kwa mwaka mzima wa fedha 2025/26 ukitarajiwa kuandikisha wanachama wapya 447,523, wakiwemo 316,957 kutoka sekta rasmi na 130,566 kutoka kwa wananchi waliojiajiri.

Bw. Mshomba alisema hadi kufikia 30 Septemba 2025, idadi ya wanachama wachangiaji imeongezeka na kufikia 1,703,821 ikilinganishwa na 932,112 waliokuwepo Juni 2021, sawa na ongezeko la asilimia 82.79, huku makusanyo ya michango yakiongezeka kutoka TZS bilioni 1,171.97 hadi TZS bilioni 2,718.87, na thamani ya Mfuko kufikia shilingi trilioni 10.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com