Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VURUGU ZA UCHAGUZI ZATAJWA KUTOKUWA SULUHISHO, HUHATARISHA UCHUMI NA MAISHA

  



Vurugu za uchaguzi zatajwa kutokuwa suluhisho, huhatarisha uchumi na maisha


Mtaalamu wa masuala ya jamii, Dkt. Francis Daudi, ametoa onyo kali kuhusu athari mbaya za vurugu zinazojitokeza wakati wa chaguzi, akisisitiza kwamba "vurugu zinazojitokeza katika chaguzi nyingi duniani huwa hazileti suluhisho la kudumu, bali husababisha athari zinazodumu kwa muda mrefu."


Dkt. Francis ambaye ni mwanahistoria alifafanua kuwa ghasia wakati wa uchaguzi huathiri moja kwa moja shughuli za kiuchumi za taifa. Alieleza, "vurugu wakati wa uchaguzi huwazuia wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali, hali inayosababisha kudorora kwa uchumi kuanzia ngazi ya mtu mmoja mmoja hadi taifa kwa ujumla."


Mbali na kudorora kwa uchumi, Dkt. Francis alieleza kuwa athari za vurugu hizo ni pamoja na upotevu wa maisha (vifo), hasa kwa wale ambao ni nguzo na tegemeo katika familia na jamii. Alisisitiza kuwa hali hiyo hupelekea familia zilizoachwa kuingia katika umasikini, utegemezi, na kupoteza nguvu kazi – mambo ambayo huacha makovu ya kijamii yanayodumu.


Maoni ya Dkt. Francis yamewafanya wananchi wengi kutumia majukwaa ya mitandaoni kuunga mkono wito wa amani na utulivu. Baadhi ya maoni yaliyoonekana kuunga mkono ujumbe huo ni pamoja na:


@mussa.lameck_ alisisitiza umuhimu wa kushughulikia mizizi ya matatizo kabla hayajageuka kuwa vurugu, akisema, "Haitakiwi watu kuachwa na vitu moyoni hadi vitoke kwa kufanya vitendo vya kihalifu, tuilinde Amani yetu kwa kuzingatia mahitaji na sauti za wananchi maskini kwa wakati."


@cdekibua alipongeza vijana kwa kuepuka kuchochewa, akisema, "Amani imeshinda... Vijana wa Tanzania tumethibitisha kuwa nguvu yetu kubwa si vurugu, bali busara, umoja na upendo kwa taifa letu." Alihitimisha kauli yake hiyo na hashtag ya NCHIKWANZA.


@bulugumagege alitoa wito wa kitaifa akisema, "Ni Kweli Kama Taifa Tuendelee Kuwa Wamoja Na Kuitunza Amani Yetu Ili Tuweze Kusonga Mbele Kams Taifa."


Ujumbe huu unaotokana na majadiliano yaliyotokea katika Jukwaa la Wachambuzi unaongeza uzito katika mijadala inayoendelea nchini kuhusu jinsi ya kudumisha utulivu wa kisiasa na kuimarisha ushirikishwaji ili kuepuka athari za ghasia katika mzunguko wa uchaguzi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com