Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC SENYAMULE AWAOMBA VIONGOZI WA DINI, WANANCHI KUTIMIZA WAJIBU WAO KATIKA KULINDA AMANI



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewataka wananchi na viongozi wa dini kuyaweka mbele maombi na kutimiza wajibu wao katika kulinda amani, hasa katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na taarifa za uwezekano wa machafuko siku ya Desemba 9.

Pia Mkoa wa Dodoma umezichagua siku tatu za Desemba 7,8 na ,9 Kwa ajili ya kufanya maombi.

Akizungumza leo Desemba 5,2025 wakati wa kufungua kikao cha maombi kilichowakutanisha viongozi mbalimbali wa dini katika Ofisi za Mkuu huyo, Senyamule amesema kila mtu ana jukumu la kuhakikisha nchi inabaki kuwa tulivu na salama.

"Kila mmoja ana wajibu wa kulinda amani. Kila mtu atimize wajibu wa jukumu lake. Wakati huu sio wa kungoja tarehe 9 itakuwaje; tusilale leo ili kuzuia 9 iwe salama," alisema.

Amesisitiza kuwa viongozi wa dini wana mchango mkubwa katika kuhamasisha umoja, maelewano na kutuliza mioyo ya wananchi, hivyo hawapaswi “kulala usingizi” katika kipindi hiki cha taharuki.

"Hapo tutakuwa tumetimiza wajibu wetu. Sisi kama Serikali tunajitahidi, nawashukuru sana,huu ni wakati wa kushikana na kuongelea lugha ya amani," ameongeza.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wananchi kuendelea kumuomba Mungu ili Taifa libaki kuwa la utulivu na mshikamano.

Kikao hicho cha maombi kilihudhuriwa na viongozi kutoka madhehebu mbalimbali ya dini, ambao walitumia nafasi hiyo kuombea amani ya nchi na kuhimiza wananchi kutohamasishwa na taarifa zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Akizungumza pia wakati wa kufunga maombi hayo amesema wanaotaka uvunjifu wamekuwa na nguvu kubwa hivyo wanaotaka amani kwa maridhiano wanatakiwa kuendelea kupaza sauti.

"Tusilale tuendelee kupaza sauti tufanye majukumu ya dini lakini kubwa tuendelee kupaza sauti Kwa hizi siku tatu,"amesema Mkuu huyo wa Mkoa.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com