Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Richard Raphael Masele
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Desemba 5,2025 Masele amesema Watanzania wanapaswa kutanguliza uzalendo na busara, na kuendelea kuchapa kazi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa badala ya kujiingiza kwenye vurugu zinazochochewa na watu wenye maslahi binafsi, wakiwamo wanaoishi nje ya nchi.
Amesema ni muhimu wananchi kuendelea kutunza nchi, kuepuka kuchezea amani ya Tanzania, na kutekeleza maridhiano kwa utaratibu wa kitaifa bila kushinikizwa, akibainisha kuwa vurugu husimamisha shughuli za kiuchumi na husababisha mateso kwa wazazi, watoto na wananchi wasio na hatia.
Masele ameonya kuwa kufanya maandamano tarehe 9 Desemba, kama kunavyoenezwa mtandaoni, kunaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii.
Masele amesema kukubali kushawishiwa kuandamana ni kujiletea hasara, kwani madhara hayo “yanawagusa wazee wetu, watoto, ndugu na majirani,” na kwamba Watanzania hawapaswi “kuichoma nchi yao, kwa sababu tukiharibu tunajihujumu sisi wenyewe.”
Amesisitiza kuwa amani ni zawadi ya pekee ambayo nchi nyingi zimepoteza kwa kushinikizwa, na baadaye zimejuta kwa gharama zilizowapata.
Ameeleza kuwa tangu aingie madarakani, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametekeleza mambo makubwa katika sekta mbalimbali, hivyo anastahili kuungwa mkono na kupongezwa, si kupigiwa debe vurugu zinazolenga kumchafua.
Masele amesema madai ya Katiba Mpya hayapaswi kutumiwa kuhamasisha machafuko, kwani “mchakato wake utaendelea kwa utulivu, si kwa vurugu zinazotengeneza mgawanyiko.”
Ameikumbusha jamii madhara ya maandamano ya siku za uchaguzi yaliyosababisha vifo na uharibifu wa mali kwa baadhi ya wananchi, akiwataka Watanzania kutorudia makosa hayo kwa kushawishiwa na watu wanaoishi nje ya nchi ambao “hawapendi kuona amani ikidumishwa.”
Amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kusimamia maendeleo makubwa katika sekta za afya, elimu, umeme na miundombinu, na kwamba vijana wanapaswa kutumia fursa zinazotolewa, ikiwemo mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, ili kujikwamua kiuchumi na kuijenga Tanzania yenye ustawi na maelewano.





Social Plugin