-𝐘𝐚𝐬𝐡𝐢𝐤𝐚 𝐦𝐤𝐨𝐧𝐨 𝐊𝐢𝐭𝐮𝐨 𝐜𝐡𝐚 𝐄𝐫𝐢𝐜k 𝐌𝐞𝐦𝐨𝐫𝐢𝐚𝐥 𝐌𝐨𝐫𝐨𝐠𝐨𝐫𝐨
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia timu yake ya wanamichezo wanaoshiriki mashindano ya SHIMMUTA 2025 wametembelea Kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu cha Erick Memorial mkoani Morogoro Disemba 4, 2025.
Timu hiyo ya NEMC ilipata fursa ya kutembelea, kufariji na kuwapa misaada ya vyakula na vifaa vya usafi pamoja na kutoa elimu ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira ikiwa ni sehemu ya kuienzi siku maalumu ya walemavu ambapo duniani kote hufanyika tarehe 3 Disemba ya kila mwaka.
Akizungumza kwenye kituo hicho kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Afisa Utumishi Mkuu wa NEMC Bi. Shukrani Haule amesema Baraza linaendelea kushirikiana na watu wa makundi yote katika kuhakikisha Mazingira yanakuwa safi na salama kwa watu wote, lakini pia kihakikisha makundi haya yanawezeshwa na kujumuishwa katika maamuzi yanayozingatia Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini.
"Baraza katika kutekeleza majukumu yake linashirikiana na watu wote na kundi hili la watu wenye ulemavu limekuwa likilizingatiwa siku zote katika mipango yake yote" Amesema Bi. Shukrani.
Naye Mtendaji wa Taasisi hiyo ya Erick Memorial, Bw. Robert Mkalawa ametoa wito kwa Taasisi za Serikali kuona umuhimu wa siku hii kama ambayo NEMC imefanya.
"Tunashukuru kutembelewa Taasisi inayohusika na Mazingira ambao ni NEMC na hii inadhihirisha kuwa hakuna Mazingira bila watu na watu wenyewe ndio sisi bila kubagua, lakini nitoe rai kwa Taasisi nyingine za Serikali kuiga mfano wa NEMC katika kuadhikisha siku hii ya Walemavu Duniani". Amesema Bw. Robert.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Michezo NEMC Bw. Fortinatus Patrick amesema kilichofanyika ni muendelezo wa kile alichokisisitiza Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi katika kuweka Mazingira wezeshi kwa makundi yote kujumuisha jamii za watu wenye ulemavu katika kuhifadhi Mazingira nchini.








Social Plugin