Na Mwandishi wetu, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema ni budi kwa kila mtanzania kuhakikisha anahimiza upendo na umoja nchini sambamba na kudumisha amani na kuheshimu sheria za nchi badala ya kuendekeza maandamano, vurugu na uvunjifu wa amani jambo ambalo limekuwa halina faida kwa Taifa, zaidi kuleta maumivu tu kwa baadhi ya Watanzania.
Dkt. Samia ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania Jijini Dodoma kwenye Viwanja vya Gwaride, mara baada ya kuibuka kinara katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 ambapo katika hotuba yake amesisitiza umuhimu wa amani nchini na kuonya kuhusu wanaoshawishi na kuratibu ghasia na uvunjifu wa amani uliojitokeza katika baadhi ya Mikoa kwa lengo la kuharibu upigaji kura wa Jumatano Oktoba 29.
"Hatuba budi kuhakikisha tunahimizana umoja na upendo kwa nchi yetu. Tunadumisha amani na kuheshimu sheria za nchi. Kinyume cha hayo maandamano, vurugu na uvunjifu wa amani husababisha maumivu na havileti manufaa wala faida kwa yeyote yule.
Niwasihi Watanzania, tuchague hekima badala ya ghadhabu, busara badala ya mihemko, upendo badala ya chuki, uvumilivu badala ya Vinyongo, umoja badala ya mgawanyiko na amani badala ya vurugu,ni wajibu wetu pia kuchagua Unyenyekevu badala ya kiburi na huruma badala ya hasira." Amesisitiza Dkt. Samia.
Dkt. Samia amesisitiza kuwa Tanzania ni moja na hakuna aliye na nguvu kuliko Taifa akibainisha kuwa kipimo cha demokrasia si ushindi katika uchaguzi Mkuu bali namna ambavyo Taifa linaweza kuendesha mambo yake mara baada ya uchaguzi Mkuu, akisema Taifa litakuwa na nguvu zaidi pale sauti zote zitakaposikilizwa na kuheshimiwa sambamba na kuponya maumivu ya baadhi ya Watanzania, akisema ni wajibu wa Kila mmoja na Taasisi zote kuifanya kazi hiyo vilivyo.
Katika hatua nyingine Dkt. Samia amewashukuru pia Viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali nchini kwa kuhimiza amani na upendo kabla, wakati wa upigaji kura na hata baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi Mkuu wa Tanzania, akiagiza shughuli zote za kijamii na kiuchumi kurejea katika hali yake kwa kuwahakikishia Watanzania amani na usalama wao.

Social Plugin