Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezindua rasmi semina maalum ya siku tatu kwa waandishi wa habari kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Pwani, Morogoro na Zanzibar, yenye lengo la kuongeza uelewa na umahiri katika kuripoti masuala ya uchumi na fedha nchini.
Akifungua semina hiyo jijini leo November 19,2025 Jijini Dodoma, Meneja wa Huduma za Kibenki na Sarafu wa BoT Nolasco Matuli amesema kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili waweze kuelewa kwa undani majukumu ya Benki Kuu, sera za fedha, mzunguko wa uchumi, usimamizi wa sekta ya fedha na namna taarifa sahihi za kifedha zinavyoweza kuchochea maendeleo ya taifa.
Amesema mafunzo hayo yatachochea uwezo wa waandishi kufasiri takwimu na sera za fedha ili kutoa taarifa sahihi, wazi na zenye tija kwa umma ikiwa ni pamoja na kuwezesha kuelewa majukumu, muundo na taratibu za BoT, ikiwa ni pamoja na jinsi inavyodhibiti mfumuko wa bei, kusimamia mabenki, na kusimamia sarafu ya nchi.
"Tunatarajia kuwa mtajenga uandishi wenye weledi katika masuala ya uchumi, hususan katika kipindi ambacho taarifa sahihi za kifedha zina mchango mkubwa katika maamuzi ya sera, biashara na ustawi wa jamii ," ameeleza na kusisitiza kuwa ;
Mafunzo haya pia yataimarisha mahusiano kati ya BoT na vyombo vya habari, kwa kuweka mazingira ya mawasiliano ya mara kwa mara ili kuongeza uwazi na upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wananchi, "amesema
Meneja Msaidizi wa Uchumi wa BoT – Tawi la Dodoma, Shamy Chamicha, ameeleza kwa kina muundo wa Taasisi hiyo na wajibu wake katika uchumi wa taifa kwa kueleza kuwa ina jukumu la kudhibiti na kusimamia sera ya fedha ili kuhakikisha thamani ya shilingi inabaki kuwa thabiti na mfumuko wa bei unakuwa katika kiwango kinachokubalika.
Chamicha amesema kuwa sera ya fedha ndiyo injini inayowezesha uchumi kukua kwa kasi bila kujenga misukosuko ya kiuchumi.
"BoT ina jukumu la kusimamia mfumo wa kifedha, ikiwemo utoaji wa leseni kwa mabenki, usimamizi wa taasisi za fedha, ufuatiliaji wa mifumo ya malipo na kuhakikisha usalama wa amana za wananchi,uthabiti wa sekta ya fedha ni msingi muhimu wa uchumi imara, " ameeleza
Chamicha amefafanua kuwa Benki Kuu pia inahusika katika kusimamia na kudhibiti usambazaji wa sarafu nchini, kuhakikisha inatosheleza mahitaji ya wananchi, ni halali, salama na yenye ubora na kwamba inaendelea kufanya maboresho ya mifumo ya malipo ili kuongeza ufanisi, kupunguza gharama na kuunga mkono ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
Akizungumzia mfumo wa utekelezaji wa Sera ya Fedha unaotumia riba na faida zake, Chamicha amesema kuwa BoT hutumia mfumo huo kudhibiti mzunguko wa fedha kwenye uchumi ili kuhakikisha bei za bidhaa na huduma zinabaki katika viwango vinavyokubalika.
Ameeleza kuwa riba ni chombo muhimu katika kusimamia mwenendo wa uchumi kwa kuwa inapoongezwa, hupunguza kasi ya mikopo na matumizi, jambo linalosaidia kupunguza mfumuko wa bei.
Meneja huyo ameeleza kuwa, viwango vya riba vinapopunguzwa, uwezo wa watu kukopa huongezeka, biashara huongeza uzalishaji na mzunguko wa fedha unaimarika, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi.
Aidha, alifafanua kuwa kupitia utekelezaji wa sera ya fedha, Benki Kuu huangalia pia faida za mabenki na taasisi za fedha, kwani viwango vya riba huathiri moja kwa moja uamuzi wa taasisi hizo kutoa mikopo, uwekezaji wao, na hali ya ushindani katika soko la fedha.
Amesema kuwa BoT hufanya tathmini za mara kwa mara ili kuhakikisha mabenki yanatoa huduma kwa viwango vinavyowezesha uchumi kukua bila kuhatarisha uimara wa sekta ya fedha.
"Mfumo huu wa sera ya fedha unaohusisha riba husaidia kupunguza hatari za kiuchumi, kuongeza uwazi katika soko la fedha na kuweka mazingira salama ya upatikanaji wa mikopo kwa wananchi, wafanyabiashara na sekta binafsi, " Amesema
Semina hiyo inaendelea jijini Dodoma kwa siku tatu kuanzia leo November 19 hadi November 21 ambapo waandishi wa habari wanatarajiwa kupata mafunzo ya kina juu ya uchumi mpana, masoko ya fedha, usimamizi wa sera na tafsiri ya takwimu za kiuchumi.






Social Plugin