

Na Kadama Malunde – Shinyanga
Shule ya KOM Primary School imeandika historia nyingine ya mafanikio katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba (PSLE) 2025, baada ya wanafunzi wake wote kufaulu kwa daraja la juu na shule hiyo kujipatia Daraja A (Bora).
Takwimu kutoka Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) zinaonesha kuwa kati ya wanafunzi 67 waliofanya mtihani, 62 wamepata Daraja A na 5 Daraja B, bila hata mmoja kupata alama za chini. Hali hii imeifanya shule hiyo kuwa miongoni mwa shule bora zaidi kitaifa, kwa wastani wa ufaulu wa 272.98.
Kati ya wanafunzi hao, wasichana 28 wamepata alama A na 4 alama B, huku wavulana 34 wakipata alama A na 1 alama B — ishara ya mafanikio ya pamoja kwa jinsia zote mbili.
Kwa miaka kadhaa sasa, KOM Primary School imejipambanua kama kitovu cha ubora wa elimu mkoani Shinyanga na Tanzania kwa ujumla, ikijenga msingi imara wa maarifa, maadili na ubunifu kwa watoto wake.
Wazazi na walezi wameendelea kuisifu shule hiyo kwa huduma bora za ufundishaji, nidhamu, na mazingira salama ya kujifunzia yanayochochea ufaulu.
Kwa matokeo haya ya mwaka 2025, KOM Primary School imedhihirisha kuwa bado ipo kileleni katika kuzalisha vipaji vinavyoipeperusha vyema bendera ya elimu bora nchini.
Hongera KOM Primary School – Kila Mwanafunzi ni Mshindi! 🏆📚
Social Plugin