Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI NDUMBARO APIGA KURA APONGEZA UTULIVU NA UHAMASISHAJI WA WANANCHI SONGEA

Waziri wa Katiba na Sheria daktari Damasi Ndumbaro akiwa anapiga kura katika kituo alichojiandikisha leo mapema katika mtaa wa Mjimwema A Songea Mjini 

 Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma 

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, ameambatana na familia yake kupiga kura katika kituo namba moja cha Mjimwema A, eneo ambalo amekuwa akipigia kura kwa miaka mingi. 

Akizungumza mara baada ya kupiga kura, Dkt. Ndumbaro amesema amefika kutimiza haki yake ya kikatiba ya kuwachagua viongozi, na amepongeza muitikio mzuri wa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi hilo muhimu la kidemokrasia.

Ameeleza kuwa katika eneo la Mjimwema A kuna jumla ya vituo tisa vya kupigia kura na wananchi wamejitokeza kwa wingi, huku mchakato ukiendelea kwa amani na utulivu.

 Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa mji wa Songea una jumla ya vituo 500 vya kupigia kura, na baada ya kupiga kura wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku za kujiletea maendeleo katika hali ya usalama na utulivu.

Aidha, Waziri Ndumbaro amewahimiza wananchi ambao bado hawajapiga kura kujitokeza kutimiza wajibu wao wa kikatiba, huku akiwataka waliomaliza kupiga kura kuendelea na shughuli zao kwa amani. 

Kwa upande wake, Zakaria Ngonyani, mkazi wa Mtaa wa Mjimwema A, amesema ameridhishwa na maandalizi na mwenendo mzima wa zoezi la upigaji kura, na amepongeza hatua ya kuongeza vituo vingi vya kupigia kura, jambo lililorahisisha ushiriki wa wananchi wengi zaidi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com