Na Mwandishi Wetu , Dar
Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salama , Albert Chalamila, amewaonya wananchi na wamiliki wa mitandao ya kijamii wanaopanga kuzima data au kueneza taarifa za upotoshaji siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025, akisema serikali imejipanga kuhakikisha mawasiliano yote yanaendelea bila usumbufu.
Akizungumza wakati wa kikao cha maandalizi ya uchaguzi mkoani humo, Chalamila amesema baadhi ya watu wamekuwa wakipanga mikakati ya kuzima mitandao au kueneza hofu kwa wananchi kupitia mitandao ya kijamii, jambo ambalo amesema halitavumiliwa hata kidogo.
“Kuna watu wanasema eti siku ya uchaguzi watazima data, wengine watakata network,nawaambia mapema, tutawafanya ‘network zisome’ hakuna kuzima data Tanzania.
Serikali ipo kazini kuhakikisha wananchi wote wanapiga kura kwa amani na wanapata taarifa sahihi muda wote,” amesema kwa msisitizo.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na vyombo vya ulinzi na usalama imeweka mifumo madhubuti ya kudhibiti upotoshaji, udukuzi na majaribio yoyote ya kuvuruga amani kupitia mitandao.
“Huu ni uchaguzi wa amani, wa maendeleo,tume ya Uchaguzi imejipanga vizuri, wasione kama wanaweza kuchezea mfumo wa nchi. Tutakuwa macho masaa 24,” amesema Chalamila.
Ametumia nafasi hiyo kuwataka vijana kutumia mitandao ya kijamii kwa kutoa elimu, hamasa na ujumbe wa amani badala ya kueneza hofu au maneno ya uchochezi.
“Vijana ndio mtaji mkubwa wa taifa. Badala ya kuzima data, wasambaze taarifa za amani, ushiriki wa uchaguzi na umoja huo ndio uzalendo,” ameongeza.
Kauli ya Chalamila imeungwa mkono na wadau wa amani na demokrasia mkoani humo, waliotaka viongozi wote wa kisiasa na kijamii kuendelea kuhimiza utulivu kuelekea siku ya uchaguzi mkuu.

Social Plugin