Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Padri Camillus Aron Nikata wa Jimbo Kuu la Songea, ambaye pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) Mwanza, amepatikana akiwa hai katika mashamba ya Kijiji cha Mawa, Kata ya Hanga – eneo alikozaliwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma, Padri Nikata amepatikana tarehe 17 Oktoba 2025 akiwa amedhoofika kutokana na njaa baada ya kukosa chakula kwa siku kumi, akishindia karanga na maji.
Taarifa ya awali ya kupotea kwake ilitolewa na Polisi tarehe 9 Oktoba 2025, na mara baada ya hapo upelelezi wa kina ulianza kufanyika kwa kushirikisha makachero waliobobea.
Upelelezi wa Polisi umebainisha kuwa sababu ya Padri Nikata kujificha kwa siku hizo ni msongo wa mawazo uliotokana na matatizo mbalimbali ya maisha.
Imeelezwa kuwa alikuwa akilalamika kuhusu madeni makubwa yaliyomlemea, hali ya kiafya pamoja na msukosuko wa mahusiano ya kimapenzi.
Inadaiwa kuwa Padri huyo alikua akimuhudumia mpenzi wake wa miaka tisa kwa kiasi kikubwa cha fedha, ambapo kati ya mwezi Juni na Septemba mwaka huu alitumia takribani shilingi milioni 39.1 kutoka katika akaunti yake ya benki ya CRDB kwa ajili ya kumgharamia mwanamke huyo, ambaye baadaye alimwacha.
Aidha, Padri Nikata amekuwa akiumwa presha ya macho na tayari alikuwa amefanyiwa upasuaji wa jicho moja huku akisubiri kufanyiwa jingine, lakini alikosa fedha za matibabu kutokana na matumizi makubwa aliyokuwa amefanya.
Pia taarifa zinasema alikuwa ameomba kuachana na huduma ya upadri kutokana na sababu za kiafya, kifedha na kiakili, lakini hakusikilizwa na uongozi wake wa Kanisa.
Kwa sasa hali yake inaendelea kuimarika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma – Songea (Homso), huku Jeshi la Polisi likithibitisha kuwa hakutekwa bali alijificha yeye mwenyewe kutokana na msongo wa mawazo uliotokana na changamoto hizo.

Social Plugin