Chama cha Skauti Tanzania kimeendesha mafunzo maalumu kwa viongozi wa Skauti kutoka mikoa tisa ya Kanda ya Ziwa, ikiwemo Shinyanga, Tabora, Simiyu, Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Kigoma na Katavi, kwa lengo la kuwajengea uwezo katika masuala ya utawala bora, uongozi, ukuaji wa wanachama na matumizi ya mfumo wa kidigitali wa kanzi data ya Skauti nchini.
Mafunzo hayo yamefanyika
leo, Ijumaa Oktoba 17, 2025, katika Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHYCOM),
yakihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, Jeshi la Polisi pamoja na
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa mafunzo hayo, Kamishna wa Skauti Mkoa wa Shinyanga, Mussa Chama, amesema lengo ni kuwajengea viongozi hao
misingi imara ya uzalendo, kujituma na uongozi wenye maadili, sambamba na
kuhamasisha kila shule nchini kuwa na klabu za Skauti ili kukuza roho ya
kujitolea kwa vijana.
“Tunataka kila kijana wa
Kitanzania awe na moyo wa uzalendo na kujitolea. Kupitia Skauti, tunawajenga
vijana kuwa viongozi bora wa kesho na raia wema wanaotumikia taifa lao kwa
heshima na uadilifu,” amesema Chama.
Kwa upande wake, Kamishna
Mkuu Msaidizi anayeshughulikia Utawala Bora Makao Makuu ya Skauti, Fredrick Nguma,
amesema chama hicho kwa kushirikiana na wakuu wa shule kimeanza mikakati ya
kuhakikisha kila shule inakuwa na angalau wanachama 100 wa Skauti,
ikilinganishwa na wastani wa sasa wa wanachama 30 hadi 50 kwa shule.
“Tunataka kuona kila shule
inakuwa na kikundi imara cha Skauti. Hii itasaidia kukuza nidhamu, ushirikiano
na uongozi miongoni mwa wanafunzi,” amesisitiza Nguma.
Akitoa pongezi kwa chama
hicho, Afisa kutoka Jeshi la Zimamoto na
Uokoaji Mkoa wa Shinyanga,
Geofrey Mwambungu, amesema Skauti wamekuwa msaada mkubwa
katika matukio ya uokoaji na kutoa huduma za kijamii wakati wa majanga mbalimbali.
Aidha, Mjumbe wa Bodi ya Skauti Mkoa wa Shinyanga, ambaye pia ni askari polisi wa Kata
ya Ukenyenge Wilaya ya Kishapu, Insp. Amini Mgata, kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Shinyanga SACP Janeth Magomi, amesema Jeshi la Polisi limeendelea
kushirikiana kwa karibu na Skauti katika kuendesha kampeni za kupinga ukatili,
kuhamasisha usalama wa jamii na kuzuia uhalifu mashuleni.
Akihitimisha mafunzo hayo
kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Afisa Elimu Sekondari wa
Mkoa, Samson Hango,
ameipongeza Skauti Tanzania kwa kuanzisha mfumo wa kidigitali wa usajili wa
wanachama ambao utarahisisha utunzaji wa takwimu na ufuatiliaji wa maendeleo ya
vijana.
“Mfumo huu wa kidigitali ni
hatua kubwa ya kimaendeleo. Unasaidia kujua idadi halisi ya wanachama, maeneo
yao na shughuli wanazofanya. Hii ni njia sahihi ya kujenga uwajibikaji na
uongozi bora katika chama,” amesema Hango.
Mafunzo hayo yamehitimishwa kwa washiriki kuahidi kuendeleza elimu waliyopata kwa viongozi na vijana wa Skauti katika mikoa yao, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kuimarisha uongozi na ushiriki wa vijana katika maendeleo ya jamii.





















Social Plugin