
Na Michael Abel, Shinyanga.
Serikali kupitia Wizara ya Nishati imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa kitaifa wa umeme jua unaotekelezwa katika wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, ambapo hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 78.5.
Mradi unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 325, unatekelezwa na kampuni ya Sinohydro kutoka nchini China, na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2025.
Akizungumza leo Oktoba 14, 2025 mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema serikali imeridhishwa na hatua zilizofikiwa, na kwamba kukamilika kwake kutasaidia kufikia malengo ya ajenda ya kimataifa ya nishati endelevu kwa wote ifikapo mwaka 2030.
“Tumefika kujionea utekelezaji wa mradi huu na kiukweli nimeridhishwa na kasi ya utekelezaji ambayo mkandarasi amekuwa akienda nayo mpaka sasa. Mradi huu ni sehemu ya jitihada za Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma ya nishati safi, salama na nafuu. Kukamilika kwake kutaongeza upatikanaji wa umeme vijijini na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati visivyo rafiki kwa mazingira,” amesema Mhandisi Mramba.
Kwa upande wake, Mhandisi msimamizi wa mradi huo, Emmanuel Anderson, amesema kasi ya ujenzi imeongezeka baada ya changamoto kadhaa zilizokuwa zikisababisha ucheleweshaji kutatuliwa, na kwamba mkandarasi yuko katika hatua za mwisho za utekelezaji.
“Changamoto za awali kama ucheleweshaji wa vifaa na mvua nyingi sasa zimedhibitiwa. Mkandarasi anaendelea kwa kasi nzuri na matarajio yetu ni kuona mradi unakamilika kwa muda uliopangwa,” amesema Mhandisi Anderson.
Naye Meneja wa Kampuni ya Sinohydro, Eng. Daniel Xu, amesema kampuni yake imejipanga kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa ubora unaohitajika na ndani ya muda uliowekwa.
“Tumeongeza nguvu kazi na vifaa kuhakikisha tunamaliza kazi hii kwa wakati, tunathamini ushirikiano mzuri tunaoupata kutoka serikalini na wananchi wa Kishapu tunaahidi kukamilisha mradi huu kwa viwango bora,” amesema Eng. Xu.
Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza uwezo wa nchi katika kuzalisha umeme wa nishati jadidifu, kusaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa taasisi, viwanda, na wananchi, sambamba na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika mkoa wa Shinyanga na taifa kwa ujumla.
Mhandisi msimamizi wa mradi huo, Emmanuel Anderson, akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba akizungumza mara baada ya kutembelea mradi huo.














Social Plugin